October 4, 2017

Eti samaki hawasahau - Utafiti.

samaki
Mtu huambiwa ana akili ya kusahau kama samaki. Lakini sasa huenda hilo likabadilika baada ya wanasayansi kugundua kwamba, kinyume na imani hiyo, baadhi ya samaki wanaweza kuhifadhi taarifa kuhusu mazingira waliomo kwa takriban wiki mbili.

Watafiti kutoka chuo kikuu cha MacEwan, waliwazoezesha baadhi ya samaki wa Kiafrika wajulikanao kama cichlids, kuingia katika eneo maalum la tangisamaki ili kupata chakula.

Walitolewa na siku kumi na mbili baadaye walirudishwa tena ndani ya tangi samaki hilo, na saamki hao walionekana kuipendelea sehemu hiyo maalum waliokuwa wakipewa chakula.

 Baadhi ya samaki wanaweza kukumbuka mazingira yao kwa muda wa wiki mbili
Watafiti hao wanasema ongezeko hilo la muda wa samaki kukumbuka, huenda likampa samaki nafasi ya kuishi zaidi hususan wakati kuna upungufu wa chakula.

"Samaki wanaoweza kukumbuka mahali chakula kilipo, wana uwezo wa kuishi zaidi kuliko wale ambao hawakumbuki," alisema mwandishi mwenza wa ripoti ya utafiti huo Trevor Hamilton, ambaye ni mwanasayansi wa chuo hicho kikuu cha MacEwan nchini Canada,

Alisema samaki wanaweza kukumbuka kwamba sehemu maalum ina chakula bila kuwepo tishio la samaki wanaoweza kuwaua, na hivyo wataweza kurudi tena katika sehemu ile.

Wanasayansi hao wanasema samaki wakiwa baharini, ni muhimu waweze kutambua maeneo yalio na chakula ili waweze kuendelea kuishi.