October 10, 2017

Mambo 3 ya kukusaidia kutawala hisia na mawazo yako juu ya hofu uliyonayo.

1: Kubali kwa 100% kuwa una hofu.
Mtu yoyote anayetaka kutoka kwenye kifungo cha aina yoyote ile huwa ni rahisi sana kutoka kama kwanza atakubali na kukiri wazi kuwa yeye ni mfungwa kamili. Hauwezi kuchomwa sindano au kupewa vidonge na daktari ambaye hajakupima na kuhakikisha kuwa wewe ni mgonjwa na unaumwa ugonjwa fulani. Ili daktari aweze kukutibu vizuri kabisa ni lazima ahakikishe unaumwa kwa kukupima na kufahamu hakika huyu mtu ni mgonjwa.

Jambo kama hili linajitokeza hivyo hivyo katika matibabu ya hofu. Ni lazima ujipime wewe mwenyewe binafsi na kuhakikisha una hofu ndani yako juu ya jambo fulani kisha uamue badae kwa dhati kuondokana na hofu hiyo. Kubali wazi kuwa una hofu iliyomo ndani yako kisha uanze kutafuta namna (process) ya kuiondoa hofu hiyo. Hauwezi kuwa huru kifungoni kama unajiona mfalme. Kubali wewe ni mfungwa kwa sasa ili uwe mfalme badae.

2: Fahamu chanzo cha hofu yako uliyonayo kimeanzia wapi.
Usikubali kuondoa tatizo la aina yoyote lile katika maisha yako pasipo kufahamu chanzo cha tatizo husika kimeanzia wapi. Kama ukiliondoa tatizo hilo pasipo kufahamu chanzo chake ni rahisi sana tatizo hilo kurudi na kuendelea kukutesa. Fahamu mizizi na chanzo cha tatizo lako kisha weka uamuzi wa dhati wa kukabiliana na tatizo husika.

Angalia ni wapi hofu yako inapotokea, angalia ni nini asili na chanzo cha hofu yako. Je, hofu yako inatokana na hisia au mawazo yako binafsi uliyonayo, yaani nikimanisha chanzo cha hofu yako kinatokea ndani yako binafsi? Je, hofu yako inatokana na mazingira yaliyokuzunguka na mambo yaliyokutokea huko nyuma? Au hofu yako inatokana na mambo unayokutana nayo ofisini, kazini, barabarani au vitu vilivyokuzunguka kila siku? Amua kutafuta chanzo cha hofu yako kisha amua kwa dhati kuikabili hofu hiyo kwa kila namna usiku na mchana.


3: Amua kwa dhati kuondokana na hofu uliyonayo kwa kubadili chanzo chake cha taarifa.
Usizani ni kitu rahisi kuamua kuondoa kitu kilichomo ndani yako kama hutoweza kuamua kwa dhati kutoka ndani yako kwa asilimia mia moja. Unahitaji uwe na ufahamu na maarifa ya kutosha ya kukusaidia kukabiliana na hali halisi ya kitu unachohofia kutoka ndani yako. Maarifa na ufahamu ndio kitu cha kwanza kinachoweza kukupa msaada wa kuishinda hofu iliyojaa akilini mwako.

Kwa mfano watu wengi sana hapo nyuma katika nchi yetu walikuwa na hofu ya kuwekeza katika soko la Hisa la Dar es salaam (DSE) kwa sababu ya uoga wa kupoteza fedha zao wanazowekeza. Na hii ilitokana na taarifa mbaya walizowahi kusikia hapo nyuma kutoka kwa watu walioshindwa au kutokuwa na maarifa ya kutosha hata kufikia kuwapa na wengine hofu (sumu ya maneno) ndani yao na muathilika mmojawapo nikiwa ni mimi. Baada ya watu wachache kuanza kupata maarifa na taarifa mpya juu ya uwekezaji wa aina hii na kuanza kuwekeza kwa faida, basi na wengine wakaanza kukimbilia na kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kuanza kuwekeza ndani ya soko hili. Amua kwa dhati kutoka kwenye hofu uliyonayo ndani yako, wakati mwingine kwa kuamua kujifunza juu ya kile unachokihofia kila wakati.

Nakusihi jifunze kuwekeza katika taarifa sahihi ikibidi pasipo kusubiri watu au waandishi fulani kukuandikia bali amua mwenyewe kusoma vitabu na kusikiliza CD na DVD za mafunzo kutoka kwa watu waliofanikiwa kweli kwa vitendo na si kwa maneno matupu. Hakuna mtu anayefundisha au kuandika nje ya kile alichojifunza kwa watu wengine aliowasoma au kuwasikiliza na kwa kupitia maisha yake binafsi. Soma vitabu ili uweze kuvuka kila aina ya changamoto ikiwemo hofu iliyojengeka kwa muda mrefu ndani yako.