October 4, 2017

Kwanini unahitaji rafiki/marafiki wazuri.

Waswahili wanasema nioneshe rafiki zako nami nitakuambia tabia zako. Msemo huu ni wa kweli. Kila mtu ni shahidi wa usemi huu ingawa kuna baadhi hujifariji kwa kusema mimi nina rafiki jambazi lakini mimi si jambazi.

Ukweli ni kwamba tabia za watu ambao ni marafiki hufanana kwa kiwango kikubwa ingawa hazitafanana kwa asilimia mia moja kwakua kila mtu anatofautiana na mwingine kwa namna moja ama nyingine. 

Kwa mfano mtu anaweza kukutambulisha kwa rafiki yake na kusema ukimuona yeye umeniona mimi. Si kweli kuwa mtu mwingine anaweza kuwa wewe lakini kuna namna fulani au katika maeneo fulani(ambayo ni muhimu sana) mnaendana na sababu hiyo ndiyo iliyoleta ukaribu ndani yenu na kuwafanya muwe marafiki.

Mara nyingi marafiki zetu wamekua na sehemu kubwa sana ya kutufanya tufikie au tusifikie malengo yetu. Marafiki hawa tunaweza kuwa tumeonana nao mahali pa kazi,masomoni, mahali tunapoishi, sehemu za ibada. N.k

Marafiki wanafaida sana katika malengo yetu ikiwa ni kututia moyo pale tunapokata tamaa, kutushauri, kuturekebisha wakati tunapokosea, kutufariji, kushirikiana nao nyakati za huzuni na furaha na pia marafiki ndiyo hao wanaoweza kuwa mume au mke baadae. Kwa hiyo marafiki wanamchango mkubwa sana katika maisha yetu ya kila siku.

Kuna baadhi ya watu hushindwa kufikia malengo ya maisha yao waliyojiwekea kwasababu tu ya marafiki walionao. Marafiki hawa huwa ukuta wa wao kufanya mambo mazuri na makubwa wanayohitaji kuyafanya. Ni vizuri kuwa makini na kuchunguza vizuri kama maraki tulionao wana chembechembe za mambo ambayo tumeyapa kipaumbele. 

Kama una rafiki mlevi, mtembezi, anayependa kubishana, mvivu na wewe ukawa na tabia za tofauti na yeye basi urafiki wenu waweza kuingia doa au hapo lazima mmoja abadilike amfuate mwingine ili muweze kuongea lugha zinazofanana.