October 20, 2017

Ujue mzunguko wa hedhi, siku za hatari na salaama.

Mzunguko wa kawaida wa hedhi ni siku 28 – 32. Kama zitakuwa chini ya siku 28 hadi 24 basi huo ni mzunguko mfupi na kama zitakuwa zaidi ya 32 -35 huo ni mzunguko mrefu.

Ili kujua mzunguko wako ni mrefu au ni mfupi ni LAZIMA upate wastani wa mizunguko yako ya hedhi ya miezi mitatu.


Namna ya kuhesabu
1- Anza kuhesabu mzunguko wa hedhi yako kuanzia siku ya kwanza umepata hedhi yako.
2- Na kisha malizia na siku moja kabla ya kupata hedhi nyingine ya mwezi mwingine.
3- Mfano umepata hedhi leo tarehe 8 basi nenda katika kalenda yako andika siku ya kwanza, kisha subiria mpaka unapopata hedhi nyingine, kama utapata hedhi nyingine tarehe 06 mwezi wa saba mana yake mzunguko wako wa hedhi umeisha tarehe 05 mwezi wa 7 na ni mzunguko wa siku 28.
4- Baada ya hapo tafuta wastani wa mzunguko wako kwa miezi yako mitatu yaani mwezi wa 6-7, mwezi wa 7-8 na mwezi wa 8-9.

Ili tuelewane vizuri tutatumia mzunguko wa wastani wa siku 28 ambao umegawanyika katika makundi matatu.
 – Siku za hedhi 
– Siku Kupata Mimba 
– Na Siku Zisizokuwa za Kupata Mimba.


1- Siku yako ya kwanza ya mzunguko wako wa mwezi ndio siku ya kwanza ya hedhi
Siku za hedhi au SIKU ZA DAMU katika mzunguko wa siku 28 huwa ni 4-5. Hesabu kuanzia siku ya kwanza umepata hedhi mpaka siku ya mwisho ya kutokwa damu. Zinakuwa siku 4 hadi siku 5 lakini zinaweza badilika. 

2- Baada ya kumaliza siku 4-5 za damu, siku ya 6 hadi 10 NI SIKU AMBAZO kupata mimba NI VIGUMU, ingawa inaweza kutokea ukapata ujauzito.

Pia siku ya 19 hadi siku ya 28 ni siku ambazo sio rahisi au tuseme kwa ujumla haiwezekani kupata ujauzito

3- Siku ya 11 hadi ya 18 ni siku zenye UWEZEKANO MKUBWA wa kupata mimba. Katika siku hizi kama wewe unatafuta mtoto na huna matatizo yeyote ya kiafya basi inafaa kuongeza bidii katika tendo la ndoa ili kuongeza uwezekano wa kupata ujauzito.

Kawaida ukipata hedhi basi jua ya kwamba yai lako liliokuwa limekomaa limekosa mbegu ya kiume hivyo ule ukuta uliokuwa umejengwa na damu kwa ajili ya kupokea mtoto na kumkuza umebomoka…. Baada ya hapo mwili unaanza kuandaa yai lingine la mwezi unaofuata.

NOTE 1 – Tangu yai kutoka katika mfuko wake linaweza kukaa masaa 12 hadi siku 2 likiwa bado linauwezekano wa kurutubishwa na mbegu ya kiume na kuanza kuunda mtoto. 

NOTE 2 – Mbegu za kiume zinaweza kaa siku 3 hadi siku 7 zikiwa na uwezo wa kurutubisha yai la uzazi.