December 9, 2017

Mkeo anakosa hamu ya tendo la ndoa? Msaidie hivi

Leo ningependa kuzungumza na wanaume ambao wapo kwenye ndoa lakini wanasumbuliwa na tatizo la wenzi wao kupoteza hamu ya tendo la ndoa. Sanaa ya mapenzi ni pana sana, ndani yake kuna changamoto nyingi ambazo unapaswa kuwa na upeo wa ziada kuweza kuzitambua na kupambana nazo.

NINI HUSABABISHA WANAWAKE KUKOSA HAMU YA TENDO LA NDOA?
Wanaume wengi wanapoingia kwenye ndoa, akili zao huzielekeza kwenye urahisi wa kupata haki yao ya ndoa muda wowote wanaohitaji kufanya hivyo.

Wanaamini kwamba wanawake wapo kwa ajili ya kuwaburudisha na inapotokea wakakumbana na hali tofauti, ikiwemo ya mwanamke kukosa utayari na msisimko wa tendo, huanza kufikiria tofauti kwamba huenda wameanza kusalitiwa.

Ukosefu wa maarifa ndiyo unaosababisha hali hii, kwamba mwanaume anaamini muda wote atakaojisikia kuwa na mkewe faragha, bila kujali utayari wa mwenzake, basi mwanamke hatakiwi kuwa na kipingamizi chochote.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Dr. Sheryl Kingsberg, mshauri wa mapenzi na mtaalamu wa saikolojia ya uhusiano, kati ya asilimia 50-70 ya wanawake waliopo kwenye ndoa, huwa wanabakwa na waume zao.

Kwa tafsiri nyepesi, wanaingiliwa kimwili na waume zao bila kuwa na utayari lakini wanashindwa kukataa kutokana na mila na tamaduni zao.

Zipo sababu nyingi zinazosababisha tatizo la kukosa hamu ya tendo kwa wanawake. Msongo wa mawazo unatajwa kuongoza kwa kusababisha tatizo hili. Pia migogoro ya kimapenzi, matatizo ya homoni na kutoridhishwa kimapenzi, ni sababu nyingine zinazotajwa kuchangia mwanamke kupoteza msisimko na hamu ya kuingia faragha na mwenzi wake.
Hata hivyo, sababu huwa hazifanani kwa kila mmoja, kila mwanamke ana sababu iliyomfanya akafikia hatua ya kukosa hamu ya tendo la ndoa na kama asipopata ushauri wa kitaalamu, au kuzungumza na mwenzi wake kurekebisha tatizo hilo, hali huzidi kuwa mbaya kiasi cha kusababisha ndoa nyingine kuvunjika.

DALILI ZAKE NI ZIPI?
Zipo dalili za wazi na nyingine za kificho ambazo huashiria kwamba mwenzi wako amepoteza msisimko na hamu ya tendo akiwa na wewe. Yawezekana kila siku wewe ndiye unayemuanza mkiwa faragha na usipomuanza, basi siku itapita kimyakimya. Hiyo ni dalili ya kwanza. Dalili nyingine kubwa ni kuhisi maumivu makali wakati wa tendo.

Ukiziona dalili hizi, na nyingine nyingi zikiwemo kila siku kusingizia anaumwa tumbo au kichwa ili usimguse, basi ujue kuna tatizo hapo na badala ya kuwa mkali au kumhisi kwamba huenda anachepuka, unapaswa kumsaidia ili arudi kwenye hali yake ya kawaida.

NINI CHA KUFANYA?
Kama nilivyosema awali, zipo sababu nyingi zinazosababisha hisia za mwanamke kuisha na kupoteza kabisa hamu ya kukutana faragha na mwenzi wake. Ili kukabiliana na tatizo hili, ni vizuri kuanza kushughulikia sababu zilizomfanya mwenzi wako akafikia kwenye hatua hiyo mbaya.

SHUGHULIKIA MIGOGORO YA KIMAPENZI
Endapo kuna tatizo limetokea kati yako na mwenzi wako, kwa mfano mwenzi wako anahisi unamsaliti kwa kutoka na mwanamke mwingine, humshirikishi kwenye mipango ya familia, hajui hata mshahara wako ni kiasi gani na unatoka lini, unaleta ubabe ndani ya nyumba, unachelewa kurudi nyumbani bila sababu, humtoi ‘out’ wala humnunulii zawadi, atahisi humpendi.

Atabaki na vinyongo na manung’uniko ndani ya moyo wake na taratibu ataanza kupoteza hisia za mapenzi juu yako. Ni lazima kila mgogoro unapotokea, ukashughulikiwa kwa busara ili kila mmoja aridhike na kuondoa dukuduku ndani ya moyo wake.

Wanawake wengi ni mahodari wa kukaa na vinyongo ndani ya mioyo yao hivyo kama mwanaume hujui namna ya kumaliza kabisa matatizo, umpendaye ataishia kwenye hali ya kupoteza hamu ya kuwa na wewe faragha. Mpe nafasi mwenzi wako azungumze hisia zake na hiyo itamsaidia kutoa vinyongo na manung’uniko.

MSAIDIE KUPAMBANA NA MSONGO WA MAWAZO
Njia nzuri ya kupambana na ‘stress’ zinazosababishwa na kazi, ni vizuri wanaume kuwa wanaelewa nini wenzi wao wanahitaji wanapotoka kazini.

Hii inawahusu zaidi wanawake wanaofanya kazi kwani wengi wao wanaongoza kwa kupoteza hamu ya tendo kutokana na matatizo wanayokutana nayo kutwa nzima wakiwa kazini.

MRIDHISHE MUWAPO FARAGHA
Sababu nyingine inayosababisha mwanamke kupoteza hamu ya kushiriki tendo la ndoa na mwenzi wake ni mwanaume kushindwa kumridhisha wanapokuwa faragha.

Narudia tena kusema kwamba mapenzi ni kama sanaa nyingine yoyote ambayo ni lazima ujifunze ili uwe hodari. Huwezi kujua kupiga gitaa na likatoa muziki mzuri kama hukujifunza, vivyo hivyo kwenye mapenzi.

Wanaume wengi wana tatizo la kushindwa kuwafikisha wenzi wao wawapo faragha na kwa bahati mbaya zaidi, wengi hawapo tayari kujifunza. Wanaishi kwa mazoea, wanashiriki tendo kwa namna ileile, hakuna ubunifu, hakuna kujifunza na matokeo yake, wanasababisha wenzi wao wakose msisimko wa kuendelea kushiriki nao.

Ndiyo! Atafurahia vipi kuwa na wewe faragha wakati anajua kwamba utamuacha njiani baada ya kumaliza haja zako na hutashughulika kwa chochote kuhakikisha na yeye anafurahi?

Ni muhimu kwa wanaume kujifunza namna ya kuwafurahisha wenzi wao wawapo faragha ili kudumisha uhusiano imara. Ni matumaini yangu kwamba mpaka hapo, wanaume watakuwa wamepata kitu cha kujifunza.

MFANYIE MAMBO MAZURI
Mbinu nyingine ya kumsaidia mkeo kama amepoteza hamu ya tendo ni kuwa na utaratibu wa kumfanyia mambo mazuri. Wanandoa wengi wakishaoana, wanaona kama wameshamaliza kila kitu. Wanaacha kufanya yale mambo yote waliyokuwa wanayafanya awali ambayo ndiyo yaliyosababisha wenzi wao wakawapenda.
Mfanyie ‘sapraizi’ mkeo kwa kumnunulia zawadi mara kwa mara, hata kama ni ndogo kiasi gani.
Tenga muda wa kuwa naye hata kama ratiba zako zinakubana kiasi gani na pale unapopata muda, mtoe ‘out’. Mambo haya japo unaweza kuyaona kama ni madogo, lakini husaidia kwa kiasi kikubwa kuamsha upya hisia za mapenzi.Tazama video: Mtoto anavyoumbika tumboni tangu siku ya kwanza hadi anapozaliwa.