January 30, 2018

Fahamu Kabila nchini Tanzania ambalo mwanaume hutoa gobore kama mahari.

Mara nyingi tumezoea kuona mwanamke anapoolewa mahari ambazo hutolewa ni ng’ombe, mbuzi, fedha au vitu vingine vya kawaida ambavyo hutumika katika jamii kila siku, lakini kwa wakazi wa Mkoa wa Katavi wao hali ni tofauti.

Mwanaume wa Kabila la Wapimbwe waishio wilayani Mlele mkoani Katavi wanapooa hulazimika kutoa gobore kama sehemu ya mahari kwa wazazi wa mwanamke.

Mmoja wa wazee wa kabila hilo akielezea sababu ya kudai gobore kama sehemu ya mahari ni kwa sababu kabila hilo shughuli yao kubwa ni uwindaji, hivyo kudai gobore katika mahari ni ili kujiongezea zana za uwindaji. Aidha alisema kwa sasa hali hiyo imepungua kutokana na sheria kali za uwindaji na umiliki wa silaha.

Utamaduni huu umefanya silaha kuzagaa kwa wingi wilayani huo hali ambayo inatishia usalama wa wananchi pindi yanapozuka mapigano. Kwa mwaka jana Jeshi la Polisi lilifanikiwa kukamata magobore 40 na silaha nyingine kama vile SMG.