January 10, 2018

Kompyuta za Mac na simu za iPhone zina kasoro - Apple.

Apple wamesema kwamba simu zote za iPhone, iPad na kompyuta za Mac zimeathiriwa na kasoro kubwa ambayo imegunduliwa katika kifaa muhimu ndani ya mitambo hiyo.

Ilibainika wiki iliyopita kwamba kampuni za teknolojia zimekuwa zikifanya juu chini kutatua kasoro ambazo zimepewa jina Meltdown na Spectre, ambazo zinaweza kuwapa wadukuzi fursa ya kuiba siri na habari muhimu kutoka kwa simu na kompyuta.

Kasoro hizo zinapatikana katika kisilikoni ambacho ndicho huendesha shughuli ndani ya kompyuta au simu wakati inapofanya kazi.

Mabilioni ya kompyuta, simu na tabiti kote duniani zimeathirika. Apple nao pia wamethibitisha kwamba simu zao na kompyuta pia zimeathirika.

Kampuni hiyo imetoa vipande kadha vya programu vya kusaidia kuziba kasoro za Meltdown. Apple wamesema hakuna ushahidi wowote kufikia sasa kwamba kasoro hizo zimetumiwa na wadukuzi.

Hata hivyo, wamewashauri wateja kwamba wanafaa kupakua vipande hivyo vya programu kutoka kwa mitandao ya kuaminika kuepuka kupakua programu ambazo zinaweza kuwa na kirusi.