January 12, 2018

Lugha 5 za upendo, we unaongea ipi? jifunze hapa

Moja ya tatizo kubwa katika kuonesha upendo (love) tumeshindwa kufahamu kwamba mke na mume huongea lugha tofauti za upendo. Kila mmoja huwa na namna tofauti jinsi anavyojisikia unampenda kwa mfano mwingine ukimpa zawadi yoyote hujisikia unampenda na ukimsifia anaona ni maneno matupu na mwingine ukimsifia basi hujiona raha na hujisikia unamthamini na kumpenda.

Kuonesha upendo kuna lugha kama zilivyo lugha za mawasiliano na utamu wa lugha ni pale unapoifahamu kwa kuisikia na kwa kuiongea, pia utamu wa upendo katika ndoa au mahusiano ni pale unapofahamu lugha ya upendo kati yako na mpenzi wako.

Itakuwa vigumu sana kwa anayejua kibena kuanza kuongea na anayejua kimasai na wote wakawa wanadhani inawezekana. Kumbuka Babeli haikujengwa ikaisha kwani baaada ya lugha kuharibiwa kila kitu kilisambaratika.

Kimsingi ili kuelewana na mpenzi wako kuna lugha za msingi tano ambazo kati ya hizo moja wapo inaweza kuwa ni maalumu kwa ajili ya mpenzi wako na kuifahamu au kuzifahamu lugha zake basi unaweza kujenga mahusiano imara. Hata hivyo mahusiano bora huanza kwanza na Hofu ya Mungu (Christ in you)

Lugha tano muhimu ambazo mara nyingi wapendanao hutumia ni:

1. KUWA NA MUDA NA MWENZI WAKO (Quality time)
Msingi wa kuwa na muda na mwenzi wako ni upamoja (togetherness) kimawazo, kimwili na kiakili. Kukaa na kuangalia TV pamoja si kuwa na muda na mwenzi wako kwani hapo mnaipa TV qulity time.

Kuwa na muda na mwenzi wako ni kukaa pamoja na kumpa attention yote, anaongea na wewe unamsikiliza tena ninyi wawili tu. Ni kutembea pamoja yaani mmeamua kwenda kutembea kwa ajili ya kwenda kutembea wewe na yeye tu si kwa sababu mnaenda kanisani au mnaenda kazini.

Kupeana muda wa pamoja ni kama vile kwenda kula pamoja (outing) ninyi wawili na mkifika hapo kwenye hoteli mnaongea kwa kuangaliana ninyi. Kama mpenzi wako yupo kwenye hili kundi yaani kwake kupendwa ni kuwa pamoja basi ni dhahiri ukifanya haya mara kwa mara atajisikia raha sana na atajisikia unampenda sana.

Hata hivyo kama mpenzi wako kwake lugha ya upendo ni zawadi ataanza kulalamika why unakuwa na mimi tu muda wote hata zawadi huniletei? Maana kwake kupokea zawadi ndio kuonesha unampenda na si kufuatana kila mahali.

2. KUPEANA ZAWADI (Receiving gifts)
Zawadi ni kitu chochote unachoweza kukishika kwa mikono na kinakupa hisia kwamba aliyenipa zawadi alikuwa ananifikiria na ananipenda.

Zawadi huelezea upendo kwamba alikuwa ananiwaza na kuniona mtu wa maana sana kwake. Wanandoa wengi hupuuza na kuona kwamba zawadi siyo kitu muhimu katika mapenzi, pia wapo wengine hudhani zawadi kwa mpenzi hadi kiwe kitu kikubwa kama gari au nyumba, vitu vidogo sana kama pipi, Chocolate au maua ni zawadi za msingi sana na zina maana kubwa sana katika kuimarisha mapenzi katika ndoa.

Zawadi ni muhimu, pia na uwepo wako pale mke wako au mume wako au mpenzi wako anakuhitaji anapokuwa na shida (wapo wakiona shida hukimbia wapenzi), uzoefu inaonesha zawadi hata za kutoa muda wako hukaa katika kumbukumbu za mhusika kwa miaka mingi bila kusahau na pia huongeza level ya mapenzi kwako.

Inawezekana mke wako au mumeo ni watu ambao akipewa zawadi basi yeye ndio kupendwa yaani ndio anaguswa zaidi, moyo wake unaamini ukipewa zawadi ndio unapenda. Kama mpenzi wako kupewa zawadi ndio lugha yake ya upendo basi ikitokea wewe unampa sifa kwa mambo mazuri anafanya usishangae akikwambia punguza maneno zawadi zipo wapi? Atakwambia anataka matendo si maneno!

3. MGUSO (physical touch)
Kukumbatia, kubusu, kushikana mikono na sex (katika ndoa) ni njia ya mawasiliano ya hisia za upendo au kupendwa. Watafiti wengi hasa wa maendeleo ya watoto wamethibitisha kwamba kukumbatia, kumbusu na kumshika mtoto kunampa afya njema kihisia.

Inawezekana mume wako au mke wako kwake kupendwa ni kukumbatiwa au kupata busu kabla hujaondoka asubuhi na unapokutana naye tena baada ya shughuli za kujenga familia au kutembea mmeshikana naye mikono, pia inawezekana kwako ni jambo gumu na unaona kama ushamba fulani hivi au ulimbukeni.

Jambo la msingi fahamu kwamba kila mmoja wetu ana aina ya kujisikia anapendwa na ni kitu kidogo lakini kinaweza kufanya ndoa au mahusiano yako kuwa matamu au machungu.
Unaweza kutumia muda mwingi kumpikia chakula kitamu, au kununulia zawadi ya gharama, hata hivyo kama mwenzi wako kupendwa ni kupokea mguso wa kimwili bado zawadi zako hazitamkuna vizuri kama ungempa mguso wa kimwili.

Katika milango ya mitano fahamu, kugusa ndiyo peke yake kunahusisha mwili mzima. Kuona tunatumia macho, kunusa tunatumia pua, kusikia tunatumia masikio, kuonja tunatumia ulimi lakini kugusa ni mwili mzima.

4. KUSAIDIANA KAZI
Hii ni kufanya vitu ambavyo mke wako au mume wako anatarajia au anategemea ungefanya kuonesha unampenda na kumjali na kuwa wewe na yeye ni kitu kimoja.

Inawezekana anategemea ungemsaidia kutandika kitanda, kusafisha nyumba, kupika, kufua nguo, kumsafisha mtoto, kuosha gari, kufyeka majani.

Kwa kumsaidia katika majukumu yake yeye anaona kwamba unampenda kuliko watu wote duniani, hivyo ndivyo aina hii ya watu walivyo.

5. MANENO YA SIFA
Je ni mara ngapi umesema Asante au kumsifia mpenzi wako kwa jinsi alivyofanya kitu ambacho kilionekana kizuri?

Na je kawaida unapomsifia kwa vile alivyo au anavyofanya huwa anajisikiaje?
Hayo maswali ni ya msingi sana mtu kujiuliza hasa kama unataka kujua mwenzi wako kwake maneno mazuri ya sifa ndiyo KUPENDWA.

Fahamu kwamba wewe ndiye mtu muhimu kuliko mtu yeyote duniani kwake, hivyo maneno unayoongea yanamjenga au yanambomoa na si kubomoa tu bali na kumuumiza na unampa wakati mgumu.

Lengo la upendo si kulalamika kwa kile ambacho hupati bali ni kufanya kile ambacho kitamsaidia yule unayempenda, yule umechagua uishi naye hadi kifo kitakapowatenganisha.

MWISHO
Itapendeza sana na utaona mabadiliko makubwa sana pale utakapotambua njia bora ya kuonyesha upendo kwa mwenzi wako, pale utakapoelewa lugha ya mwenzi wako ni pia ili muweze kuelewana vizuri zaidi.