January 23, 2018

Mambo sita(6) Muhimu kujua kabla hujanunua ardhi/kiwanja au shamba.


Mambo sita(6) Muhimu kujua kabla hujanunua ardhi/kiwanja au shamba.


Kila mtu ana haki ya kumiliki mali kwa mujibu wa ibara ya 24 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Ardhi ni mali hivyo ni lazima uitunze na uimiliki kisheria.

Ni Watanzania wengi wanamiliki ardhi. Pia ni wengi ambao wana kesi kwenye mabaraza ya ardhi na mahakamani kuhusu ardhi. Wengine wamedhulumiwa fedha au kula hasara kwa kununua ardhi bila kujua mambo muhimu ya kuangalia.

Ni wengi wamenunua ardhi inayomilikiwa zaidi ya mtu mmoja. Wengine wamekuwa wakiuziwa na mtu ambaye siyo mmiliki. Benki na taasisi nyingi za kifedha zimejikuta zikitoa mkopo zaidi ya mmoja eneo moja.

Mnunuzi makini hayumbishwi na bei ya kiwanja au nyumba kiasi cha kushindwa kuzingatia mambo ya msingi kabla ya ununuzi. Mwingine anakwepa gharama za kuwatumia mawakili katika ununuzi, wanakimbilia kununua kiwanja au eneo matokeo yake wanaishia mahakamani. Kwa bahati mbaya kesi za ardhi mara nyingine zinachukua zaidi hata ya miaka kumi.

Ardhi ni nini?

Ni eneo lote la sura ya dunia na chini yake isipokuwa madini na mafuta ikiwa ni pamoja na mimea yote inayoota juu yake, majengo na vitu vyote ambayo ni vya kudumu juu ya ardhi, hii ni kwa mujibu wa sheria ya ardhi na. 4 ya mwaka 1999.

Nani mmiliki wa ardhi kisheria? Kwa mujibu wa sheria za nchi ardhi ni ya Watanzania wote, ipo chini ya Rais kama msimamizi tu (Trustee) anayesimamia mambo ya ardhi kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi.

Kila mtu ana haki ya kumiliki mali kwa mujibu wa ibara ya 24 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Ardhi ni mali hivyo ni lazima uitunze na uimiliki kisheria.

Mambo ya kuzingatia kabla ya kununua ardhi


1. Itambue ardhi yenyewe unayonunua (On-site search)

Hii ni hatua ya kwanza kabisa, tembelea eneo unalotaka kununua ili ujue unauziwa eneo gani, ikiwa ni pamoja na ukubwa wa eneo, mipaka pamoja na hali ya eneo kiujumla, ujue eneo liko bondeni, kilimani au eneo lolote.

2. Usipende kutumia mtu kununua ardhi, 

Ni vizuri ukakagua eneo lako. Nilishawahi kukuta mtu ana kesi huko Kibaha alinunua eneo akijua ni ekari nne, kwenda kuangalia ni heka mbili na aliyeuza hana mamlaka ya kuuza.

3. Thibitisha umiliki, 

Hii ni hatua ya pili. Unaweza kupata jibu la hili kwa kuuliza majirani husika wa eneo hilo kwa muda wako mwenyewe.

4. Usiwe kipofu kwa maneno ya muuzaji, 

Udogo wa bei au maneno ya dalali, pia kama eneo halina hati ya kisheria ulizia kwa serikali ya mtaa au ya kijiji kama kuna hati ya kimila. Fuatilia ujue eneo hilo haswa linamilikiwa na nani, siyo unakurupuka tu na matokeo yake unakuta watu wanne mnauziwa eneo moja, mnaishia mahakamani wote.

5. Fanya utafiti kwa msajili wa hati juu ya umiliki (Search), 

Pia unaweza kuthibitisha umiliki kwa kufanya maulizo kwa msajili wa hati chini ya Wizara ya Ardhi, hii unaifanya kwa njia ya barua ya kawaida, Sheria ya usajili wa ardhi sura ya 334 kifungu cha 97(Kwa Tanzania) kinatoa haki kwa mtu yeyote kufanya maulizo hayo, na utajua taarifa juu ya eneo husika, kabla ya kufanya maulizo hayo uwe na namba ya kitalu ya eneo husika.

6. Usijidanganye, kununua eneo bila ya kujiridhisha kwamba hakuna mtu mwenye haki katika eneo, 

Wengi wamejikuta wananunua mali bila kujua kwamba kuna watu wengune wana haki kwenye eneo husika, mfano eneo au nyumba isiwe limechukuliwa mkopo (Mortgage), kusiwe na mpangaji (Lease) kama yupo mjue mnalimalizaje hilo suala, uwe makini kama ni mali ya wanandoa (Matrimonial property) kupata ridhaa ya mke au mume.