January 11, 2018

Sababu zinazopelekea wanaume wengi kuwa wapweke

Wanaume tangu tukiwa watoto wadogo, tunafundishwa kuwa imara, na kujikaza kiume pindi tunapokabiliana na vikwazo. Jambo ambalo linasisitizwa pia kwa nguvu kupitia kampeni mbalimbali za masoko zinazoundwa na wafanya biashara ili kudumisha chachu inayoelezea uimara wa mwanaume.

Huniamini? Fuatilia majarida yanayowahusisha wanaume na uangalie matangazo mbalimbali. Kuanzia kwenye vifaa vya usafi wa ngozi, dawa, vinywaji na hata michezo, vyote vimeshamiri dhana ya uimara wa mwanaume. Lakini je, ujumbe huu hauleti madhara zaidi kuliko mema kwa wanaume wapweke?

Chanzo cha upweke kwa vijana
Kwa hakika, ningependa kutaja moja ya chanzo kikubwa cha upweke kinachopelekea vijana wengi wapambane na changamoto hii katika jamii zetu kwa nyakati za sasa.  Chanzo ni “Uzuri na ubora wa mwanaume mbele ya wanawake” jambo ambalo limejazwa ujinga na upotofu mwingi ambao unaikabili jamii yetu kwa sasa.

Usinielewe vibaya. Nimeamua tu kuwa mwaminifu, kwasababu tatizo la uzuri na ubora mbele ya wanawake ni mojawapo ya mambo yanayowatatiza wanaume wengi, jambo ambalo huwa ninawasaidia watu wengi wanaojaribu kuunda picha ya ujasiri wao wa nje mbele ya jamii yetu.

Mimi ni mshauri ambaye nina ujuzi wa masuala mbalimbali ya wanadamu. Ukweli ni kwamba, siwezi kukuambia ni wanaume wangapi huwa nafanya mawasiliano nao na pengine kuzungumza nao ana kwa ana wakielezea huzuni, kukataliwa, na hasira juu ya hali ya maisha yao.

Ingawa habari zao zinaweza kuwa tofauti, lakini wote hushiriki ushirika wa kawaida – Upweke.

Kutoka kwa mwanaume ambaye hupigwa na mkewe lakini hawezi kufunguka na kuomba ushauri kwasababu ya kuogopa kuchekwa … kwa milionea ambaye hana rafiki kwa sababu hawezi kuruhusu urafiki kwa hofu ya usalama wake.

Wote huo ni upweke tu!
Kwa uzoefu wangu binafsi na kulingana na tafiti mbalimbali, zipo sababu kuu tano zinazopelekea wanaume wengi kuwa wapweke. Zaidi ya hayo, pia ni kwa namna gani janga hili linazidi kuwaua taratibu.

1. Wanaume huogopa kuonekana dhaifu
Unataka kujua sababu kubwa ya upweke wa wanaume – kuogopa kuonekana wadhaifu: Kwa hiyo wengi wetu tunafundishwa kwamba, kuwa mwanaume, unapaswa “kujivuta na kujisukuma mwenyewe ” pasipo kuupa moyo wako nafasi ya kukushusha au kukuangusha.

Hapa kuna shida. Baadhi yetu hatuwezi kujivuta wenyewe kwa sababu tunakabiliwa na unyogovu (depression), wasiwasi au mchanganyiko wa yote wawili. Hakuna mwanaume anataka kuonekana kuwa dhaifu. Ili kuepuka mtazamo huu, ni rahisi kuyafungia moyoni bila kubaliana na udhaifu wake.

Jambo ambalo linatuongoza kwenye sababu inayofuata.

2. Wanaume hawazungumzii kuhusu hisia zao
Hii ni moja ya sababu kubwa sana inayopelekea wanaume wengi kuwa wapweke. Na kwa bahati mbaya, imejengeka ndani ya fikra zetu tangu wakati wa kuzaliwa kwamba “wanaume halisi” hawazungumzii juu ya hisia zao.

Na unajua nini?
Wanaume wengi wangependa kuzungumza juu ya kitu chochote isipokuwa kinachoendelea ndani ya mioyo yao. Siyo kwamba hawataki. Wanataka kufanya hivyo.  Lakini kwa sababu ya fikra sumu na mtazamo hasi uliojengeka, wanaogopa kuhukumiwa na kuchekwa. Na hofu hiyo ndiyo inatuongoza kwenye sababu ya tatu.

3. Wengi huogopa kupoteza usalama wao
Jana tu, mtu mwenye umri wa kati alinitumia ujumbe wa maandishi kupitia simu yangu ya mkononi akiomba ushauri, alianza kwa kuniandikia kwamba alikuwa na upweke sana. Nilipomwuliza kama ana rafiki, alisema, “Hapana.”

Ukweli ni kwamba kila mtu ni wa pekee, lakini moja ya adha kubwa utakayoutana nayo kwa watu au mtu mpweke ni ukosefu wa urafiki wa karibu.

Huenda unajiuliza kwa nini?
Jibu ni rahisi. Kuwa marafiki na mtu – kama vile marafiki wa kweli na sio “urafiki wa uongo,” unapaswa kuikubali hatari kwa kiasi fulani. Hiyo ina maana ya kukuwa wakati mwingine utalazimika kumshirikisha rafiki yako siri na hisia zako, ikiwa kama njia mojawapo ya kupata ufumbuzi wa matatizo yako.

Lakini ukweli unabaki kuwa, sio jambo rahisi kufanywa na mwanaume na kama haukubaliani na mimi, jaribu kumuuliza mwanaume yeyote karibu yako, akuambie kama huwa anamshirikisha rafiki yake siri zake kwa lengo la kupata ufumbuzi wa matatizo yake?

4. Kuwa tofauti na wengine
Ukweli ni kwamba, uwezo wa kupigania na kufuata kile unachotaka maishani kwa msukumo wa hali ya juu ni kipaji. Ndio maana si wanaume wote wenye sifa ya kuwa wakurugenzi serikarini au katika mashirika binafsi.

Si kila mtu amezaliwa kuwa alpha. Kwa sababu ambazo hatuelewi kikamilifu, baadhi ya wanaume ni wa kawaida tu, hawawezi kujiamini zaidi kuliko wengine. Tofauti hii hupelekea athari za kifikra kwa wanaume ambao wamekosa uwezo huo, inawafanya wajisikie kama “wapochini ya watu fulani” .

Baya zaidi, badala ya kujitahidi kuishi kwa kuboresha uwezo walio jaaliwa, wanajaribu kuiga kwa kuyaishi maisha ya watu wengine na matokeo yake wakishindwa wanapondeka mioyo na hatimaye kubakia wapweke.

5. Uchache wa nafasi za urafiki
Utafiti unatueleza kwamba urafiki wa wanaume huanzia kwenye uzoefu wa pamoja na wenye nguvu. Mfano. kwenye mjumuiko wa huduma kama mafunzo ya kijeshi,  timu, chuo, au kilimo na shughuli zingine zinazohusisha jumuiya ya watu.

Swali la kujiuliza ni kwamba, Nini hutokea ikiwa hushiriki tena kwenye mjumuiko wa aina hiyo au marafiki uliowazoea wakitoweka? Ukweli ni kwamba kwa wanaume, ni tatizo kubwa.

Unachopaswa kufanya
Jiulize. Je, kuna fursa ngapi zilizopo mbele yako katika umri huu uliopo?

Kuna baadhi ya majibu na machagulio yanayoweza kufaa.

Mifano ni pamoja na kujiunga na vikundi vya mazoezi, tumia nafasi ya ujirani na (ofisini) kazini kujenga nafasi ya urafiki mpya. Ingawa ni jambo lenye changamoto kwa mwanaume aliyeishi katika upweke kwa muda mrefu. Kama unashindwa kukabiliana na tatizo lako la upweke ni busara kutafuta msaada wa kitaalamu.