January 20, 2018

Tabia 8 zitakazokufanya upendwe na jamii na ufanikiwe kirahisi.

Katika maisha kuna vitu vingi inapaswa tujifunze ili tuweze kuishi maisha yenye furaha na amani na wakati mwingine unapojua jinsi ya kufanya ili uweze kuishi na jamii inayokuzunguka inakurahisishia kupata mafanikio na kutimiza ndoto kupitia wengine leo tunatazama tabia ambazo zinaweza kukusaidia kuishi vizuri na wengine na kukupelekea upendwe na iwe rahisi kwako kufanikiwa
1. Jipende na uwapende wengine
Upendo ni kitu muhimu sana katika maisha yetu ,upendo hutuunganisha na wengine na kutufanya tuweze kusaidiana katika taabu na raha,hata hivyo  Mungu ametuagiza pia tuishi kwa upendo ” 1kor 16:14 fanyeni kila kitu kwa upendo, Jipende na kujijali,kuwa mtu nadhifu wa mwili na mavazi,kuwa makini juu ya maisha yako naya wengine .
2. Jiheshimu na heshimu wengine
Ukiheshimu wengine na wewe utaheshimiwa vilevile, jifunze kuheshimu hisia na mawazo ya wengine,tumia maneno ya busara unapokuwa unatoa mawazo yako juu ya watu wengine epuka kutoa maneno ya kuudhi na kejeli maana kejeli hutia doa hata kama ulikuwa unatoa ushauri mzuri.Onyesha heshima kwa watu wote(1peter2:17)
3. Shirikiana na jamii inayokuzunguka
Shiriki shughuli za kijamii mfano kwenye misiba na sherehe,fariji wengine wanapopatwa na matatizo,tengeneza uhusiano mzuri na majirani,ndugu na jamaa
4. Jitolee kwa ajili ya wengine
Kutoa ni ishara ya moyo safi wala si ishara ya utajiri,maana kuna matajiri wasiotoa chochote kwa wanyonge pia  kuna masikini wengine hujitolea  kile walichonacho nakugawana na  wengine ,hauwezi kuwa na thamani kwa jamii kama unahela nyingi alafu jirani yako anakufa kwa njaa, kuna watoto wa mitaani,ombaomba wasaidie na utapata Baraka kwa Mungu,hata kama si kwa kitu toa hata ushauri unaweza kumfaa mtu na baadae akakukumbuka.
5. Kuwa mshauri wa wengine
Unaweza pia kuwasaidia wengine kwa kutoa ushauri wanapokuwa wapo kwenye matatizo magumu ya maisha,kuna watu wana msongo wa mawazo(stress), kuna wakati mwingine mtu anakuwa na uhitaji mkubwa wa neno la faraja na matumaini ,yawezekana ukampa walau neno moja tu zuri nalikaweza kumfaa kuokoa maisha yake,neno moja tu zuri laweza kuwa kama kipande cha mkate kwa mtu anaekaribia kufa kwa njaa, na mtu huyo atakukumbuka katika maisha yake na utajenga urafiki na uhusiano mzuri na jamii.
6. Jiamini ili uaminike
Mafanikio mengi huja kwa kujiamini kwa maana nyinginenaweza kusema kujiamini ndiyo mlango wa mafanikio mengi kwa binadamu,kila mtu atavutiwa na wewe kama utaonekana unajiamini  katika mambo yako,ukijiamini ni rahisi kabisa kupata mafanikio,utajiri na marafiki pia.
7. Jifunze kusamehe
Kuishi na watu vizuri ni sayansi,yahitaji uelewa wa tabia za watu wanaokuzunguka na kujua jinsi gani ya kuishi nao,hata hivyo migogoro na mikwaruzano ya hapa na pale haikwepeki hata kama ungechagua kuishi na Obama,ndiyo maana tunasema hakuna binadamu aliyekamilika hata mmoja sote tunamapungufu hivyo ni lazima tuvumiliane na kusameheana  kwenye biblia pia inasemwa ,Kwa uhuru samehe wengine kama Mungu anavyokusamehe(kol 3:13 )ni kweli kuna wakati mwingine unaweza kumwekea kinyongo mtu na ukaishi nacho lakini kikawa kinakufanya uishi bila amani hivyo ikisamehe utajiepusha na stress za kuweka kinyongo zinazoweza kuharibu afya yako,ukisamehe pia unaweza kupata marafiki wa kudumu katika maisha yako.
8. Tii mamlaka na sheria
Ni picha mbaya kwa mtu ambaye mara kwa mara anapatikana na makosa mbalimbali ya uvunjifu wa sheria za nchi ,jinai au kufungwa jela,sheria zimetengenezwa kwa madhumuni mazuri ya kulinda usalama,haki na usawa miongoni mwa wanajamii,hata Mungu anatuhimiza jambo hili” Wale waliokwenye mamlaka wanapaswa kupata heshima yetu(1sam 24:1-6)  tii sheria bila shuruti.