January 1, 2018

Sisi ni WATANZANIA, sio waccm wala wachadema - Tanzania.

Kwako mpenzi, TANZANIA wa leo.

Kwenye ramani ya dunia sijawahi kuona taifa liitwalo CCM, CUF, CHADEMA ama WAZALENDO bali kuna taifa liitwalo TANZANIA. Kwa pamoja tu watanzania, Wagogo kwa Wamakonde, Wasukuma, wachaga na Wahaya n.k kwa pamoja tu watanzania.

Viongozi wa kidini, serikali, vyama vya upinzani, mahakama, vyombo vya ulinzi, wasanii na wanamichezo sisi sote ni WATANZANIA. Kwanini tuharibu hatima ya nchi yetu kama watanzania kwa maslahi ya vyetu vya kisiasa?

Huu sio wakati wa kuijenga CCM, CUF wala CHADEMA bali ni wakati wa kuijenga TANZANIA bora, TANZANIA ambayo watoto na wajukuu wetu wataifurahia na kutukumbuka sisi kama wazazi wenye busara na maarifa. 

Watanzania naomba tuachane na mambo ya ushabiki na tusimamie UKWELI na HAKI kwa manufaa ya TANZANIA yetu ya sasa na kesho. Huu ni wakati wa WANACCM na WANAUPINZANI kuungana kwa pamoja kwa HAKI na USAWA ili kulijenga taifa letu.

Tufungue masikio, tusikilizane, Tusiwekeane supa gluu midomoni, tukusanyike kwa pamoja, tuambizane na kurekebishana mapungufu yetu na mapungufu ya Taifa kwa UKWELI na HAKI kwa ajili ya kuijenga TANZANIA yetu.

Wahenga walisema umoja ni nguvu. Kama tutagawanyika huko kugawanyika kwetu ndio  kutakuwa anguko letu kama Taifa, kama hatutaisikilizana huko kutokusikilizana kwetu ndio kutakuwa anguko letu kama Taifa. 

Nguvu, akili, muda wa vikao na pesa tunazotumia kujenga vyama vyetu, kama tungeziwekeza katika Taifa letu, tungekuwa wapi kama WATANZANIA?!!.. 

Leo chama kipo, kesho je? Leo tuko chama hiki kesho tutafukuzwa ama tutahamia chama kingine, lakini kamwe hatuwezi kuondoa UTANZANIA ndani yetu, kwenye vina saba vyetu, hata tukienda Ulaya bado tunabaki kuwa WATANZANIA.

Wako TANZANIA ya kesho.