January 21, 2018

Umuhimu wa kukaribiana kihisia na mpenzi wako.

Unaweza kujiuliza, hivi inawezekana uhusiano au ndoa ikadumu pasipo wanandoa kuwa na ukaribu wa kihisia au mvuto wa kihisia baina yao?

Jibu ni kwamba wawili hawa wanaweza kuwa pamoja lakini ladha ya uhusiano wao lazima itapooza na hata kufa kama hakuna ukaribu au mvuto wa kihisia baina yao.

Mara nyingine kukosekana kwa ukaribu au mvuto huu kunaweka ufa mkubwa baina ya wawili hawa na kuongeza nafasi za wao kutengana hususani dhoruba na mawimbi yanapovuma na kuyatingisha uhusiano au ndoa yao. Uhusiano wa aina yoyote unahitaji ukaribu, bila kujali ni ukaribu wa kimwili au kihisia, na pasipo ukaribu huu kuna uwezekano mkubwa mapenzi yakanyauka.

Hapa ndipo wapenzi au wanandoa wengi hupata shida na changamoto kwenye namna ya kuhakikisha ukaribu huu hauyumbi.

Ni vyema kila mmoja wetu akaelewa kwamba ni ngumu sana kujenga ukaribu wa kimwili kama hakuna ukaribu wa kihisia. Unatamani kuwa karibu na mtu kwa sababu ndani yako unasikia msukumo huo kihisia na pia hauwezi ukawa na mvuto au ukaribu wa kihisia kama wakati wote mko mbali mbali au hamuonani kwa kipindi kirefu.

Hapa ndipo utagundua kwa nini mapenzi ya watu wengi huathirika mara mpenzi mmoja anapokuwa mbali na mwenzake hususani kwa muda mrefu.

Kama hauwezi kuwa naukaribu au mvuto wa kimwili au kihisia kwa mwenza wako, basi kamwe usitegemee kuwa na uhusiano wenye afya na yenye kudumu.

Unaweza kuniuliza kwa nini? Jibu lake ni rahisi tu; pasipokuwepo na mvuto au ukaribu wa kimwili na kihisia wanandoa mnakosa kitu cha kujishikia, au ngao ya kujikingia katika nyakati ambazo mapenzi yenu au uhusiano wenu unapitia mitikisiko.

Unakuta mtikiso mdogo tu unafanya watu waliopendana muda mrefu kutengana halafu unajiuliza, mbona kitu chenyewe kidogo hivyo? Yani walishindwa kukishuhulikia?

Wanadamu tumeumbwa na kiu ya huu ukaribu au mvuto “intimacy”. Sio kwamba unaamua ngoja niwe nao au sasa nimechoka kuwa na ukaribu huu.

Hii ni asili yetu wote na ni njaa ya kila mmoja wetu. Hii ndio maana vitendo virahisi kama vile kushikana mikono, kutekenyana, kukumbatiana au kubusiana ni muhimu sana kwenye uhusiano wenu.

Hata kama mara nyingine wengine wanazuiwa na utamaduni au imani yao, lakini mnapokuwa wanandoa na mnauhalali wa kushiriki mapenzi basi vitu hivi vinabaaki kuwa muhimu sana. Yawezekana hupendi maana hukuzoea au una mtazamo hasi lakini ni vema kufahamu kama mwenza wako anapenda ili usimyime hitaji lake.

Fahamu kwamba katika uhusiano hususani wa ndoa, kila mmoja yuko kwa ajili ya mwenzake na kila mmoja ana umuhimu mkubwa kwa mwenzake.

Kama unajua kabisa kwamba unaweza kumtazama mpenzi wako mkiwa chumbani au sehemu nyingine yenye faragha na akakurudishia alama au ya tendo au neno kwa mfano kwa kutabasamu au kukukonyeza kukuonyesha kwamba amefurahia wewe kumtazama, basi hii inaweza kuwa ngazi mojawapo ya kugundua kuwa mnaukaribu au mvuto huu kwenye uhusiano wenu.

Kama nilivyokwisha kusema awali, ukaribu huu au mvuto huu ndicho kitu kinacholiwezesha penzi kustahimili katika nyakati ngumu na kuendelea kutamani kupenda au kupendwa na wapenzi wetu.
Ukaribu na mvuto huu ninaouzungumzia ndio unaomfanya kila mpenzi kuwa na uhakika kwamba anapendwa na anatosheka na kufurahia uthamani wa penzi hilo.

Mara nyingi sana ninawauliza wateja wangu wanaokuja kwenye ushauri nasihi “counseling” hususani kwa masuala ya ndoa, nawauliza “hivi unauhakika gani kuwa mumeo au mkeo anakupenda?” Wengi hukosa majibu, wengi husema sijui au sina uhakika. Hii inaonyesha wazi kuwa ukaribu na mvuto baina yao umeathirika au umekufa kabisa ndio maana mmoja hana uhakika wa penzi la mwenzake.

Ukaribu mkubwa na wa wakati wote kwa yule uliyetoa ahadi ya kuwa naye maisha yako yote ni jambo la muhimu sana, tena jambo la muhimu kila wakati. Pasipo ukaribu na mvuto huu ile kiu au hamasa ya kuishi pamoja maisha yote inapoteza umuhimu na mara nyingine kuonekana isiyowezekana kabisa.