January 14, 2018

Zijue faida za kutumia tunda la tango kwa wingi

Tango ni tunda ambalo hujulikana sana kwa kuwa na faida ya kuondoa sumu mwilini na wengi wamekuwa wakilitumioa kwa namna mbalimbali.

Historia inaeleza kuwa tunda hili lilikuwepo na lilitumiwa sana enzi za kale katika jamii za Misri na Ugiriki. Watumiaji wake hawakuwa wakilitumia kama chakula tu, bali walilitumia kama dawa baada ya kutambua uwezo wake mkubwa wa kuilinda ngozi.

Tunda hili ambalo wengi hulitumia kama mboga lina kiwango kikubwa cha maji na ‘soluble fiber’ ambayo husaidia siyo tu kutunza mbgozi, bali pia katika kupunguza uzito wa mwili.
Zifuatazo ni baadhi ya faida za tunda la tango.

Hupunguza harufu mbaya mdomoni
Bakteria wanapokaa kwa wingi ndani ya mdomo hupelekea kuzalisha harufu mbaya. Lakini utumiaji wa tunda la tango ambalo lina wingi wa maji, kutasaidia kupunguza harufu kwani hutengeneza majimaji ya mate kwa wingi hivyo kuwaosha bakteria wote.

Huilinda mifupa
Tango lina wingi wa vitamin K ambayo huhusika sana na kuimarisha mifupa ya mwili. Imeripotiwa kuwa madhara mengi ya kuvunjika kwa mifupa ya mwili husababishwa na upungufu wa vitamin k. Hivyo utumiaji wa tango utakusaidia kuimarisha mifupa yako na kuwa mwenye nguvu.

Hukufanya kuwa mwenye afya
Kama inavyojulikana kuwa tango husafisha takataka zilizoko ndani ya mwili ambazo huweza kuwa hatari kwa afya yako kutokana na sumu zilizobeba, basi utakubaliana nami kuwa ulaji wa tunda hili kwa wingi kutakusaidia kuondoa sumu na hivyo kuwa na afya njema.

Hupunguza hatari ya kupata saratani
Tunda la tango lina wingi wa ‘lignans’ ambayo huulinda mwili dhidi ya saratani mbalimbali kama vile, saratani ya matiti, saratani ya tezi dume na saratani ya kizazi.