February 5, 2018

Aina mbili za wanaume ambazo wanawake wanapaswa kuzifahamu.

Unapotaka kuanza uhusiano na mtu, unahitaji kuwa makini kuhakikisha kuwa mtu huyo atakuwa sahihi kwako na sio mnaanzisha uhusiano kisha baada ya muda mfupi mnaachana. Kwa upande wa wanawake, kuna wanaume wa aina mbili ambao unatakiwa kuwajua kabla ya kufanya maamuzi ya kuwa nae katika uhusiano. Kuna yule atakayesema kitu akimaanisha lakini kuna mwingine atasema ili tu kukuridhisha kwa wakati huo afanikishe haja ya moyo wake.

Hapa chini ni aina za wanaume ambazo unatakiwa kuzifahamu;
Mwanaume wa kwanza atakwambia anakupenda kwa sababu anataka kulala na wewe na kisha kwenda kwa mwingine lakini kuna mwanaume atakayekwambia anakupenda akimaanisha akisemacho na kwamba anakuhitaji katika maisha yake ya sasa na ya baadae.

Kuna mwanaume atakayekufanya wewe pekee ujisikie maalumu na muhimu katika maisha yake, lakini kwa upande mwingine, kuna mwanaume atakaye kufanya wewe pamoja na wengi mjisikie wa muhimu huku akihakikisha hamjuani..

Mwanaume mmoja itamchukua muda bila kusema kuwa ninyi wawili mnafaa kuwa wachumba na hata kufunga ndoa kwa sababu anataka kuhakikisha hamfanyi makosa katika uamuzi huo, lakini mwanaume mwingine atakuwa tayari kukwambia atakuoa hata ukimuuliza siku mbili baada ya kukutana naye, kwa sababu anataka kukudanganya umuamini.

Upande mmoja kuna mwanaume atakayekuwa mtoto wa mama ambaye atakuwa anamsikiliza mama yake kwenye kila kitu, wakati upande mwingine kuna mwanaume atakayekuwa akimuheshimu mama yake lakini atasikilizana na mkewe pia.

Kuna mwanaume atakayekuwa hapendezwi na wewe na kila mara atakuwa akikusema kwa sauti kana kwamba anakukaripia hata kama mnazungumza kitu cha kawaida, wakati mwingine atakuwa akizungumza kwa upole na kwa fahari akifurahia kuwa mpenzi wako.

Kuna mwanaume atakayekuwa mcha Mungu na uhusiano wenu ataujenga katika misingi ambayo itampendeza Mungu, lakini mwingine ataonyesha kuwa anamcha Mungu ili tu akupate wewe kwa sababu anajua kwamba unataka mtu anayemcha Mungu, na baada ya kukupata wewe ndio tabia zake za kweli zitajidhihirisha.

Mwanaume wa kwanza atafanya uhusiano wenu kuwa siri kubwa, hatotaka kuambatana na wewe, hatokutambulisha kwa ndugu, jamaa wala marafiki zake, wakati mwanaume wa upande wa pili atajisikia fahari kuwa na wewe, atakutambulisha kwa ndugu zake wakujue, atatunza siri zako na kuhakikisha uhusiano wenu unazidi kuchanua.

Kuna mwanaume atakuja katika maisha yako kukupotezea muda, kukupa msongo wa mawazo, kukuharibia ndoto zako, kukukatisha tamaa wakati mwanaume mwingine akija katika maisha yako atakuja kukusaidia, kukutia moyo, kukuwezesha kupiga hatua zaidi hadi ufanikiwe kwani anaamini mafanikio yako ni yenu sote.

Mwanaume anaweza akaja kwenye maisha yako kwa ajili ya kulala na wewe tu akaishia hapo wakati unaweza kupata mwanaume ambaye atakuja kwenye maisha yako na kuwa mume, awe mwaminifu kwako na kupata watoto.

Mwanaume mmoja anaweza akawa ni kosa a muda mfupi ambalo litakusababishia maumivu ya kudumu wakati mwanaume mwingine anaweza akawa ni baraka ya kudumu ambayo itaathiri maisha yako kwa njia salama.

Ni vyema ukawafahamu kwa makini na undani kabla ya kuamua kiongia katika uhusuano.