February 8, 2018

Historia fupi ya maisha Emmanuel Mgaya (Masanja Mkandamizaji).

Maisha yake ya Utotoni
Jina lake kamili ni Emmanuel Mgaya japo wengi humfahamu kwa jina lake la Sanaa, la Masanja Mkandamizaji. Emmanuel Mgaya alizaliwa mkoani Iringa  Disemba 25, 1985.

Elimu yake.
Alipata elimu yake ya msingi na sekondari  mkoani Iringa kabla ya kwenda Dar es Salaam ambapo alisoma Utangazaji katika chuo cha Dar es Salaam School of Journalism.

Maisha yake ya Sanaa.
Alianza kuigiza tangu akiwa mdogo lakini kwake hakuweza kujua kama alikuwa na kipaji cha kuigiza kinachoweza kumuingizi fedha. Alipokuja Dar es Salaam kuna wakati alikuwa akifanya kazi ya umachinga huku akiigiza igiza kama msanii mchanga.

Maisha yake kwenye sanaa yalianza kutoa matunda mwaka 2005 alipokutana na muigizaji mashuhuri wa Tanzania, marehemu Steven Kanumba na miaka michache baadae walianzisha kundi la uchekeshaji la Ze Comedy lililoanzia kufanya kazi kwenye kituo cha runinga cha East Africa Television na baadae kuhamia katika Runinga ya Taifa (TBC) ambapo lilibadilishwa jina na kuwa Orijino Komedi. Kundi hilo linaundwa na Emmanuel Mgaya (Masanja Mkandamizaji) Mjuni Silvery (Mpoki) Lucas Mhavile (Joti) Mac Regan, Seki, Wakuvanga.

Mbali na kuwa muigizaji/mchekeshai Emmanuel Mgaya pia ni muimbaji. Tayari ametoa album yake ya nyimbo za dini inayokwenda kwa jina la ‘Hakuna Jipya’ aliyoitoa mwaka 2014. Kabla ya kutoa album hiyo, alitoa wimbo unaoitwa ‘Ugali’ mwaka 2013.

Maisha nje ya Sanaa.
Ukiachia mbali kipaji chake cha uigizaji/uchekeshaji Emmanuel Mgaya pia ni mchungaji. Mgaya ni mchungaji katika kanisa lake linalofahamika kama ‘Mito ya Baraka.’

Mbali na kuwa mchungaji, Mgaya pia ni mjasiriamali ambapo anajishughulisha na mambo mbalimbali yanayomsaidia kumuingizia kipato. Kwanza, Mgaya anajihusisha na kilimo ambapo ana mashamba makubwa ya mpunga mkoani Mbeya. Pili anamiliki mashine ndogo za kupembulia mchanga uliotoka migodini ili kuweza kutanganisha mchanga na madini na tatu, Mgaya anamiliki mgahawa wa ‘Masanja Wali Nyama’ ambapo hupikwa vyakula vya aina mbalimbali. Majuzi amefungua mgahawa mpya eneo la Kitumbini katikati ya Jiji la Dar es salaam unaoitwa Masanja Burger Point.

Familia.
Emmanuel Mgaya ana watoto wawili ambao yeye hutania amewapata ujanani.  Agosti 14, 2016 alifunga ndoa na  mchumba wake Monica.