February 17, 2018

Madhara 10 ya intaneti unayopaswa kuyafahamu katika kizazi hiki.

Katika dunia hii ya leo ni vigumu kuishi bila kutumia intaneti kwa namna moja au nyingine. Watu hutumia intaneti kuwasiliana, kupata taarifa na habari au hata  kujipatia kipato.

Kuwepo kwa intaneti kumerahisisha maisha ya mwanadamu kwa kiasi kikubwa na kufanya utendaji kazi wake uwe bora zaidi. Pamoja na intaneti kuwa na manufaa kadha wa kadha, intaneti ina athari mbalimbali. Hivyo basi fahamu madhara 10 ya intaneti.

1. Taarifa za uongo
Kila mtu anaweza kuweka taarifa kwenye mtandao wa intaneti, hivyo ni rahisi kukumbana na taarifa zisizo za kweli.

Swala hili limepelekea baadhi ya nchi na mashirika mbalimbali kujaribu kukabili taarifa mbalimbali zinazopatikana kwenye mtandao ili kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na taarifa hizo.

Ni vyema kuhakikisha tovuti au blog unayochukua taarifa inaaminika ili usije ukapotoshwa na taarifa za uongo.

2. Kichaka cha wahalifu
Wahalifu wengi hasa wale wanaotumia teknolojia hufanya uhalifu wao kwa hutumia mtandao wa intaneti au kuutumia kama kichaka chao cha kujificha.

Mtu anaweza kuwa Iran akamdukua mtu au tovuti iliyoko Marekani bila kizuizi chochote. Hivyo ni muhimu kuwa makini pamoja na kuzingatia kanuni za usalama kwenye mtandao ili uwe salama mara utumiapo intaneti.

3. Humfanya mtu kuwa mtawaliwa (addicted)
Ni rahisi mtu kuwa mtawaliwa wa mtandao wa intaneti (internet addict). Baadhi ya watu hukaa siku nzima kwenye mtandao wa intaneti au hushindwa kutimiza majukumu yao ya kila siku kwani wao kila mara wako kwenye mtandao.

Ni muhimu kuwa na kiasi katika matumizi yako ya intaneti ya kila siku ili usiwe mtawaliwa wa intaneti.

4. Husambaza picha za ngono
Picha nyingi za ngono husambaa kwa kasi kubwa kupitia mtandao wa intaneti. Hatari zaidi ni kuwa picha hizi zinaweza kupatikana bure tena kwa urahisi kwa kila mtu.

Hili limesababisha picha za ngono kuwa rahisi kufikiwa na watoto, jambo ambalo huwaathiri kimwili na kisaikolojia.

5. Kupoteza muda
Moja kati ya vitu vinavyopoteza muda mwingi ni mtandao wa intaneti. Watu hutumia muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii au kutazama video au picha mbalimbali; muda huu ungeweza kutumiwa kwenye mambo mengine yenye tija zaidi.

6. Hurahisisha udanganyifu wa kitaaluma
Mtandao wa intaneti umekuwa ni chanzo kikubwa cha udanganyifu wa kitaaluma. Wanafunzi hununua na kupakua mitihani, insha au hata maandiko mengine ya kitaaluma kutoka kwenye mtandao ili wafaulu vyema masomo yao.

Swala hili limewafanya wanafunzi wengi wasifanye bidii kwenye masomo yao pamoja na kutumbukia kwenye wizi wa kazi za kitaaluma.

7. Hubeba biashara haramu
Mtandao wa intaneti ni mfumo mkubwa sana ambao unahusisha maelfu kwa mamilioni ya kompyuta, watu, pamoja na shughuli mbalimbali.

Baadhi ya watu hutumia mtandao wa intaneti hasa sehemu ile inayojulikana kama Deep Web ili kutekeleza bishara zao haramu kama vile kuuza madawa ya kulevya, silaha, n.k.

8. Huathiri afya
Kutumia mtandao kwa muda mrefu siyo jambo zuri kwani kunaweza kuathiri afya ya macho yako pamoja na viungo vingine vya mwili.

Inakupasa kufanya shughuli nyingine au mazoezi badala ya kukaa kwenye mtandao wa intaneti siku nzima.

9. Ni chanzo cha kusambaa kwa virusi vya kompyuta
Virusi vya kopyuta husambaa kwa urahisi sana kupitia mtandao wa intaneti.

Mfano mzuri ni kirusi cha Code Red kilichoibuka mwaka 2001 na kusambaa kwa kasi sana kwa muda usiozidi wiki moja na kuweza kuathiri seva 400,000 na kompyuta milioni moja kote duniani.

10. Huongeza matumizi ya pesa
Ili uweze kutumia intaneti utatakiwa kuwa na kifaa kama vile simu au kopyuta pamoja na huduma ya mawasiliano ya intaneti — yaani data.

Hivi vyote kwa jumla vinahitaji pesa ili uweze kuvipata. Hivyo kutumia mtandao wa intaneti sana kutakuongezea gharama ya matumizi.