February 26, 2018

Sababu 7 za kwanini kila mwanaume anatakiwa kujua kupika.

1. Kuweza kula unachokitaka
Kwa njia ya kufahamu kupika unaweza kula chakula unachotaka ambacho isingekuwa rahisi kukipata hotelini au kupikiwa na mtu mwingine.

Ikiwa pia kuna aina fulani ya upishi unaipenda, basi kwa njia ya kufahamu kupika utaweza kuifanya wewe mwenyewe.

2. Kuokoa pesa
Kununua chakula hotelini au kwenye migahawa ni gharama kubwa kuliko kujipikia wewe mwenyewe. Ukifahamu kupika hutohitaji kununua mikate au chakula hotelini bali utapika chakula chako wewe mwenyewe kwa gharama nafuu.

3. Hutegemei mtu
Mwanaume anapokuwa hujui kupika, ni wazi kuwa utakuwa unamtegemea mtu mwingine ampikie; hivyo mtu huyo asipo kuwepo ni lazima upate shida.

Kwa njia ya kufahamu kupika hatakama ni vyakula rahisi, utaweza kuishi bila kumtegemea mtu. Kwa kufahamu kupika unaweza pia kuanza maisha popote bila tatizo lolote.

4. Unalinda afya yako
Chakula ulichokipika wewe mwenyewe utakifahamu vyema. Hivyo chakula unachokipika wewe utahakikisha ni salama na bora kwa ajili ya afya yako. Hili ni tofauti na vyakula vinavyoandaliwa na mtu mwingine au katika mazingira ya kibiashara kwani kwa kiasi kikubwa huandaliwa kwa lengo la kupata pesa na si kulinda afya yako.

5. Uwezo wa kuhudumia familia
Hebu fikiri mama ni mgonjwa au amesafiri, watoto wanahitaji kula na kunywa lakini baba hajui kupika; je unafikiri nini kitatokea?

Ni ukweli usiopingika kuwa utunzaji wa familia katika swala la lishe utakuwa na changamoto kama njia mbadala hazitatumiwa. Hivyo mwanaume kujua kupika kunakupa uwezo wa kuhudumia familia vyema wakati wowote bila shida yoyote.

6. Hukuongezea maarifa ya maisha
Maarifa ya maisha (life skills) ni muhimu sana katika maisha yetu ya kila siku. Mwanaume mwenye ujuzi wa kupika ni tofauti kabisa na mwanaume asiyejua kupika.

Mwanaume anayejua kupika anaweza kuandaa chakula popote na wakati wowote ambao atatakiwa kufanya hivyo bila shida yoyote.

7. Hurahisisha kupunguza uzito
Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa vyakula vya kwenye hoteli na migahawa, vinachangia kwa kiasi kikubwa kuongeza uzito wa mwili.

Hivyo ikiwa mwanaume anajua kupika, anaweza kujipikia chakula chake mwenyewe ambacho hakitaathiri uzito wake.