February 8, 2018

Ushauri wa mtaalamu wa mahusiano kwa wanandoa.

Rachel Sussman anasaidia watu walio kwenye uhusiano kuweza kukabiliana na migogoro yao ya kimahusiano. Kama mtaalamu wa masuala ya uhusiano na mshauri wa ndoa jijini New York nchini Marekani, anawasaidia wanandoa kuvuka salama kwenye misukosuko wanayopitia kama vile kutoelewana kwenye masuala ya fedha au ya kisheria, pia kwenye migogoro mikubwa kwenye uhusiano kama wivu, kuchepuka, na kudhibiti hasira.

Hata kama migogoro kwenye uhusiano inatofautiana sana, kuna ushauri mmoja ambao anapenda kuwashauri watu wanaokwenda kwake:

Tulia na umsikilize mwenzio kwanza
Wenza kuweza kusikilizana ni jambo la muhimu sana kwenye uhusiano. Kama mawasiliano kati yenu yanakuwa kama ni adhabu, kama vile kila mmoja anafanya jitihada za ziada au analazimisha ili asikilizwe, hakuna atakayeibuka mshindi kwenye hali kama hiyo.

“Raha ya uhusiano wa kimapenzi ni pale mwenza wako anapokujua zaidi ya wanavyokujua wengine,” amesema Sussman.

“Kwahiyo, kama mpenzi wako hakufahamu vizuri, kama mpenzi wako hakubaliani na wewe, kama mpenzi wako anakukosoa, unaweza kujisikia mpweke na ukaogopa hatma ya mapenzi yenu.”

Sussman amesema kwamba ni bora kusubiri kidogo na utafakari jambo kabala ya kuamua kulizungumzia. Kama wanandoa watakuwa wanafokeana mara kwa mara kwa maneno makali bila hata kufikiria wanachosema, mawasiliano baina yao yanaweza kuisha kabisa. Lakini kama utatulia kidogo, kuuliza maswali, na ubaki wazi kwenye majibu yako ndipo unaweza kujua hasa tatizo lililopo.

“Watu kwenye uhusiano wana tabia ya kuingilia mwenzie anapoongea kwakuwa anahisi kwamba yeye ndiye anastahili kusikilizwa zaidi ya mwenzie anayeongea kwa wakati huo,” amesema Sussman.