February 12, 2018

Zifahamu passport mpya za kielektroniki zilizozinduliwa nchini,

Tanzania imezindua pasipoti mpya ya kielektroniki, yenye muonekano wa Afrika Mashariki (EAC), kufuatia makubaliano ya nchi hizo kuwa wananchi wake, wawe na vibali sawa vya kusafiri nje ya nchi.

Pasipoti hiyo itasaidia kulinda usalama wa nchi hizo, kutokana na kuwa na ‘chip’ yenye maelezo yote ya mwenye pasipoti, hivyo kusaidia kubaini wahalifu na wasiotakiwa kuingia nchi fulani. Tanzania ni nchi ya tatu, kutekeleza makubaliano hayo ya Afrika Mashariki ya kuwa na pasipoti ya aina moja, hivyo kusaidia wananchi wa Afrika Mashariki kupata huduma zozote wakiwa nje ya nchi, hata pale ambapo hakuna ubalozi.

Huduma hizo watapata ikiwa kutakuwa na ubalozi wa nchi yeyote ya Afrika Mashariki kutokana na kuunganishwa kwa mtandao, utakaosaidia mwananchi anapopoteza pasipoti yake, kusaidiwa na nchi mwanachama.

Akizungumzia uzinduzi wa pasipoti hiyo na makubalino ya nchi za Afrika Mashariki, Msemaji wa Idara ya Uhamiaji, Ally Mtanda alisema mfumo wa uhamiaji mtandao, utawezesha nchi wanachama kufanya kazi kwa pamoja kutokana kwa kuunganishwa kimtandao.
Mtanda alisema utoaji huo wa pasipoti kwa njia ya kielektroniki, utafuatiwa na viza za kielektronikia (e-Visa), vibali vya ukaazi vya kielektroniki (e-Permit) na udhibiti wa mipaka wa kielektronikia (e- Border Management).

Alisema kwa sasa pasipoti hizo, zina muonekano mmoja kwa nchi zote za Afrika Mashariki, kwa lengo la kutambulika kimataifa kwa nchi zote zikiwa na rangi moja na maneno sawa, isipokuwa kwa chini itawekwa ni nchi gani.

“Rangi na muonekano ni sawa huku Tanzania ndani ya pasipoti hizo kuna alama ya Muungano, Rasilimali na Utajiri wa Tanzania pamoja na jumba kubwa la ajabu la Zanzibar, lakini kwa nchi nyingine ndani kunatofautiana kwa kuweka alama za nchi husika,” alisema Mtanda.

Aliongeza kuwa, pasipoti hiyo ina kifaa maalumu cha kumbukumbu za mhusika, hivyo kusaidia kupata msaada wa kibalozi katika nchi za EAC, ikiwa nchi fulani haina ubalozi.

Alitaja faida za pasipoti hizo mpya kuwa ni pamoja na kuwa na ‘App’ ambayo itaiwezesha kuhifadhiwa katika simu ya kisasa (smart phone), kuwezesha mwenye nayo kupata msaada wa Hati ya Dharura katika ubalozi wowote wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo. Kutokana na muonekano unaofanana na pasipoti za nchi wanachama wa EAC, itatambulisha kwa pamoja raia wa nchi hizo, hivyo kurahisisha kupata msaada wa huduma mbalimbali inapobidi.

Mtanda alitoa mfano wa msaada wa kurejeshwa nchini kupitia balozi za nchi wanachama wakati wa dharura, ikiwa sehemu husika haina ubalozi wa Tanzania. Faida nyingine ni usalama wa pasipoti hizo, ambapo ukipita mpakani utajulikana ni nani na kama hauruhusiwi kuingia nchi husika kwa sababu za kiusalama, utadhibitiwa.

“Suala la kwanza la uhamiaji mtandao ni kuimarisha ulinzi na usalama, kudhibiti mapato ya serikali na kutoa huduma kwa haraka,” alifafanua Mtanda kuhusu faida hizo.

Alisema kwa kutumia pasipoti hiyo mpya, Mtanzania au raia wa nchi hizo atakaposafiri katika nchi zenye mageti ya kielektroniki katika uwanja wa ndege (E-gate), kama amekamilisha masuala ya Visa na tiketi, atatumia passport yake kufungua mageti hayo.

Aliweka bayana kuwa pasipoti mpya ni mwarobaini wa pasipoti za Tanzania, kutumika na raia wa nchi zingine kinyume cha utaratibu, kutokana na kuwepo kwa alama za kibaiolojia, zinazomtambua kila mtu.

Faida nyingine ya kuwa na pasipoti hiyo mpya ni kurahisisha utambuzi na utunzaji kumbukumbu za raia wa nchi wanachama, wanapokuwa katika mataifa ya kigeni pamoja na kutumika katika mipango ya jumuiya.

Mtanda aliweka wazi kuwa pasipoti hizo za kielektroniki nchini, zimeunganishwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na Wakala ya Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), ili ziweze kusomeka kimtandao.

Akizungumzia utoaji wa pasipoti mpya kwa wananchi, alisema tayari wameshaanza kutoa na kuwataka wananchi kwenda kubadilisha na kupata pasipoti mpya kuanzia sasa mpaka Januari 2020, ambao ni muda wa mwisho wa kutumika kwa pasipoti za zamani.

Hivi karibuni akizindua pasipoti hizo nchini, Rais John Magufuli alisema hatua hiyo itasaidia kuimarisha ulinzi na usalama wa mipaka ya nchini, kusaidia kudhibiti ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali na kuimarisha utoaji wa huduma za uhamiaji kwa raia wa Tanzania na wageni wanaoingia na kuishi hapa nchini.

Alisema pasipoti hizo zinakidhi viwango vya kimataifa, kwa kuwa zina alama nyingi za kiusalama, na siyo rahisi kuzighushi, licha ya gharama yake kutokuwa kubwa.

Passport hizi zitapatikana kwa kila raia wa Tanzania atakayeomba, kwa gharama ya shilingi 150,000/- tofaauti na bei ya pasipoti ya zamani iliyokuwa shilingi 50,000/-.