March 31, 2018

Je! Kufanya mapenzi na mke/mume wa mtu ni kosa kisheria?

Kwa miaka ya hivi karibuni, neno kuchepuka limekuwa likitumika sana kumaanisha mwenza (mume au mke) anayejihusisha na mapenzi nje ya ndoa yake. Ina maana kuwa, kama ni mke, anafanya mapenzi na mtu ambaye si mumewe, au mume anafanya mapenzi na mtu ambaye si mkewe.

Mke au mume anapofahamu kuwa mwenzake ametoka nje ya ndoa, au amechepuka, huchukua hatua mbalimbali, ambapo ni pamoja na kuitishwa kwa vikao vya familia, kuchana, kupelekana kwa viongozi wa serikali za mitaa, kusameheana lakini wengine hufika mbali zaidi na kwenda mahakamani kufungua kesi.

Swali ambao tungependa tujiulize sote na kulipatia jibu leo, ni je! Kufanya mapenzi na mke au mume wa mtu ni kosa kisheria?

Jibu rahisi katika swali hili ni ndio, ni kesi. Lakini si kesi ya jinai ambayo inaweza kupelekea mtu kufungwa kifungo, badala yake huwa ni kesi ya madai ambayo mhusika anaweza kutaka kulipwa fidia.

Ili kuweza kupata fidia hiyo kutokana na mtu kufanya mapenzi na mke wa mume wa mtu, mhusika atatakiwa kufungua kesi ya ugoni ambapo atadai fidia ya madhara dhidi ya mtu aliyemkamata na mume au mke wake. Madai haya yanaweza kuwa kwa mke au mume aliyechepuka pamoja na yule aliyechepuka naye (wote wawili).

Mume au mke atakayekuwa amefungua mashtaka mahakamani atalazimika kuthibitisha uhalali wa ndoa yake. Ni lazima wenza hao wawe hawakuwa wameachana wakati mmoja anachepuka, pia mwanaume au mwanamke ambaye mwanandoa alichepuka naye, asiwe amedanganywa kuwa mhusika hana mume au mke.

Katika kutoka uamuzi, mahakama itaangalia kama wanandoa hao walikuwa wanaishi pamoja ama laa, na pia ijiridhishe kuwa mtu wa tatu aliyefumaniwa hakuwekewa mtego na wanandoa hao wawili.

Lakini pia, mwanaume au mwanamke asiwe ameruhusu kitendo kifanyike (condone) halafu akageuka baadae na kuanza kudai fidia (No person shall benefit from his own wrong).

Ili kesi hiyo iwe halali, lazima mume au mke awe amemfumania mwenza wake akijamiiana na mtu mwingine. Kitendo tu cha kuwaona wakibusu au wamekaa pamoja kwenye sofa au wamo chumbani au wanakumbatiana haitoshi kuthibitisha ugoni kisheria (hii inategemea pia na utamaduni wa jamii husika).

Kikubwa katika kesi ya aina hii ni uhalali wa ndoa. Ili mambo mengine yote yaweze kuendelea mbele, lazima uhalali wa ndoa yenu uthibitishwe kwanza.

Pia, huwezi kudai malipo yaleyale kupitia ugoni ambayo pia uanyadai au umeyadai kupitia talaka kama, kwa mfano unataka kutalikiana na mke ay mume wako.