March 31, 2018

Mambo 10 ya kufanya unapopitia kipindi cha kukatisha tamaa.

Kila mtu anakutana na wakati wa kukatisha tamaa kwa kuwa na changamoto ya kifedha, Ugonjwa, kimahusiano, unafukuzwa kazi, unashindwa kulipa kodi etc. Kila kampuni pia inapitia kipindi cha namna hii; mauzo yanashuka, unapoteza mteja mkubwa, benki inauza mali zako. Kiufupi ni kuwa kila mtu lazima atapitia kipindi hiki na huwezi kukwepa.

Kitu pekee unachoweza kufanya ni namna mwitikio wako utakavyokuwa (response). Kama mwitikio wako utakuwa sahihi basi utapita salama na kushinda (Upepo ambao haukuvunji basi unakuimarisha). Maisha ya mafanikio yanategemea sana jinsi utakavyokabiliana na changamoto zinazokukabili, cha kuzingatia ni kuwa unatakiwa kuweka akili yako zaidi katika kutatua matatizo na sio kufikiria matatizo. Mafanikio na uongozi hupimwa kwa uwezo wako wa kutatua matatizo.
Kitabu cha Brian Tracy cha Crunch Time kinasema kuwa ni Lazima utambue kuwa kuna uwezo ndani yako wa kutatua kila tatizo unalolikabili. Kitabu hiki kinaeleza njia kumi za kukabiliana na kipindi kigumu cha maisha yako:

Uwe mvumilivu

Una uwezo mkubwa uanowezeshwa na zaidi ya seli bilioni katika ubongo wako. Ukiwa mtulivu unaruhusu ubongo wako kufanya kazi vizuri. Badala ya kuruhusu hisia zikuendesha, tulia na uruhusu ubongo wako wako hasa sehemu inayohusiana na kutafakari na kupata masuluhisho.
Kataa kuchukua hatua ghafla wakati umekutana na wakati wa namna hii:amua kutulia na tafakari vizuri jinsi ya kukabiliana na hali hii. Tafuta unaowaamini na ushirikiane nao katika kupata ushauri na kusaidiwa mawazo.

Mara nyingi kipindi tunapokutana na hofu ya kupotezxa ama hofu ya kukataliwa tunajikuta tunaona kama vile hatuwezi kuendelea mbele zaidi. Badala ya kuruhusu hisia za hasira na kulipiza kisasi, amua kufanya maamuzi sahihi ambayo hautayajutia. Ingawa ubongo wako unaweza kuwa na mawazo zaidi ya elfu lakini unafanyia kazi wazo moja kwa wakati, na wewe una uwezo wa kuchagua wazo la kufikiriwa na ubongo wako kwa wakati huo.

Mara nyingi yale yanayoonekana hayawezekani kabisa mwanzoni,ukitulia utajikuta unapata suluhisho yake.Amua kutafuta mambo ya kujifunza katika kila kipindi cha namna hii.

Amini uwezo wako na uwe jasiri

Kila wakati tunapopitia hali za kukatisha tamaa, huwa tunajikuta tunapoteza uwezo wetu na kuamini kuwa hatuwezi kuendelea tena. Huu ni wakati wa kujisemea maneno mwenyewe ya kujipa moyo na kukataa kukata tamaa. Hata pale mambo yanapoenda vibaya wakati kila wakati unajitahidi, usikubali kuamini kuwa haiwezekani kwenda mbele, bali amini unaweza.
Fikiri na amua kuchukua hatua kutatua tatizo na usiamini kuwa hakuna unachoweza kufanya.Hakuna tatizo ambalo halina suluhisho.Usikubali hata siku moja kuamini kuwa matatizo yanakutokea peke yako.

Amua kwenda mbele

Bila kujali nini kimekutokea,amua kuwa utaendelea mbele bila kujali yaliyotokea. Maono (Vision) na ujasiri (courage) ndio kitu huwatofautisha wengi katika safari ya mafanikio. Unachotakiwa kujua ni kuwa ujasiri sio matokeo ya kutokuwa na hofu kabisa bali ni uwezo wako wa kukabiliana na hofu (Courage is not the absence of fear but the control of it). Emerson alisema namna pekee ya kukabiliana na hofu ni kufanya vitu ambavyo unavihofia, ukiweza utajikuta hauviogopi tena. Yatazame maono yako na amua kuwa hautakata tamaa kwa namna yoyote yale hadi utakapofikia.
Usiogope kuchukua maamuzi hata kama yanawagusa watu wako wa muhimu. Fanya maamuzi yatakayokusaidia kwenda mbele kwa wakati huo. Kuna aina mbili za ujasiri.
Moja ni ile ya kuanza kitu bila kuwa na uhakika kuwa kitafanikiwa huko mbele na ujasiri wa pili ni ule wa kuvumilia bila kujali.

Tafuta taarifa sahihi

Kadiri uanvyokuwa na taarifa za kutosha kuhusiana na changamoto unayopitia ndivyo unavyoweza kufanya maamuzi sahihi. Jack Welsh alisema kitu cha muhimu katika kutatua tatizo ni kujua kwanza hali halisi iliyopo kwa sasa ni ipio na sio kuangalia tu unavyotaka iwe.
Jiulize maswali?-Tatizo hapa ni lipi, lilitokeaje, kwa nini n.k Kadiri unavyopata taarifa za kutosha ndivyo utakavyojiona ujasiri wako wa kutatua matatizo unaongezeka. Wakati unatafuta taarifa sahihi, usijiruhusu kuanza kuwalaumu watu kwa matatizo yaliyopo, jikite katika kupata majibu yatakayokusaidia kutatua tataizo lililopo. Usijiruhusu kufikia hitimisho mapema kabla haujajiuliza maswali ya kutosha, usianze kuhusisha matukio bila kuwa na uhakika, fanya bidiii kupata taarifa sahihi kwanza.

Jitawale

Kila wakati tunapojikuta tuko katika hali ya kukataliwa, tumekasirishwa au tumesalitiwa na jambo Fulani huwa tunajikuta tunapata hasira na tunataka kulipiza kisasi kwa kila jambo.
Ili upite salama kipindi cha namna hii, ni lazima ujiambie kuwa wewe ndiye unayeweza kutatua tatizo lililopo. Charlie Jonson anasema haijalishi umeanguka toka umbali wa juu kiasi gani bali unaweza kuinuka na kuruka tena kiwango gani cha juu. Usikubali kuendeshwa na yale yaliyotokea, fanya kitu kinaitwa damage control (jinsi ya kukabilia na mambo yaliyoharibika tayari).

Punguza madhara zaidi

Mambo yanabadilika kila wakati na ni lazima ukubali kuendana na hali ya mabadiliko. Watu wanaofanikiwa ni wale ambao wako tayari kuendana na mabadiliko yanayotokea. Hapa inabidi utumie “zero-based thinking”-hapa unajiuliza kuwa,kama ningekuwa najua ninayoyajua kwa sasa, je ningefanya uamuzi nilioufanya? ama ningekuwa nafanya biashara/kazi ambayo nafanya sasa? Kama jibu ni hapana maana yake unatakiwa ujipange namna ya kutoka hapo ulipo kwa haraka bila kuchelewa.
Usiruhusu uendelee katika hali uliyonayo kwa muda mrefu Zaidi ya sasa. Fanya bidii kubadilisha hali uliyonayo.

Kabiliana na changamoto yako

Hakuna kitu kibaya kama kujikuta uko kwenye kipindi cha matatizo makubwa halafu huwezi kukabiliana nacho. Amini kuwa kuna suluhisho kwa kila tatizo na una uwezo wa kulitafuta tatizo hilo, usikubai kuendeshwa na tatizo lolote, unao uwezo wa kupata suluhisho.
Jenga uwezo wako wa kukabiliana na changamoto kubwa maishani kwa kujua kua zitakuja.

Fanya mawasiliano yako kwa ufanisi

Kushindwa kwingi katika maisha kunatokana na watu kushindwa kuwasiliana na watu wao muhimu kwa ufanisi unaotakiwa. Lazima ujifunze kuwasiliana na watu muhimu kweye maisha yako wakati wote. Elezea kwa watu unaowaamini kuhusiana na hali yako ngumu, usiongeze chumvi, eleza ukweli na pia waleze mambo gani umefikiria kuyafanya kutatua tatizo lako.
Hakikisha watu wako muhimu maishani wanakuwa wa kwanza kupata habari na usiruhusu wazisikie kutoka kwa watu wengine.
Kama unafanya biashara na unapitia wakati mgumu usijaribu kuficha, tafuta namna ya kuwapa taarifa wadeni wako na uwaeleze jinsi ulivyojipanga kukabiliana na hali hiyo. Usiache hadi hali imekuwa ngumu na mambo yameshindikana kabisa ndio useme. Ukifanya hivyo watakuona sio mwaminifu na utajikuta katika wakati mgumu Zaidi.

Tambua vikwazo vinavyokukabili

Ili uweze kufika unakotaka kwenda ni lazima utambue vikwazo ambavyo vinakukabili kati ya pale ulipo na kule unakotaka kwenda. Ili kufanya hivyo ni lazima ulitambue lengo lako na liwe wzi bila shaka yoyote kwako.

Jambo la muhimu ni kuandika kwa ufanisi lengo lako unalotaka kufikia kwa wakati Fulani. Ukimaliza, jiulize je kuna mambo gani ambayo yamefanya nisiwe sijafikia hadi sasa? Katika orodha utakayoipata jiulize tena; je ni sababu ipi kati ya hizi ndio kubwa kuliko zote inayonizuia kufikia lengo langu?
Mara nyingi asilimia 80 ya vikwazo tunavyopitia viko ndani yetu na asilimia 20 tu ndio huwa nje yetu. Ili kutoka hapo ulipo kwenda kule unakotaka, ni lazima utambue vikwazo vya mbele yako na ujipange jinsi ya kuvikabili.

Tumia nguvu za juu zaidi

Kwa wale ambao wanaamini biblia wanatambua kuwa nguvu hii ndio huitwa Roho Mtakatifu ambaye huwa msaada kwa watu kuwapatia suluhisho wakati wa matatizo. Napoleon Hill wakati anafanya utafiti wake kwa matajiri Zaidi ya 400 wa marekani kugundua siri ya utajiri wao alizungumza kuwa kila aliyefanikiwa kufikia utajiri usio wa kawaida lazima alieleza kuwa kuna nguvu ya ziada waliyokutana nayo na iliwasaidia. Wengine huita superconcious mind au superhuman mind, wengi walieleza kuwa iliwasaidia kupitia muda wao wa meditation n.k.
Cha kuzingatia ni kuwa kila aliyefanikiwa alihusisha mafanikio yake na msaada wa nguvu za Mungu zilizo juu ya nguvu za kibinadamu.

Hitimisho

Hakuna tatizo unaloweza kushindwa kulitatua na hakuna chanagamoto itakayokufelisha bila wewe mwenyewe kukubali kufeli. Hata changamoto uliyonayo wakati unasoma ujumbe huu inajawabu lake. Ukweli ni kuwa utakutana na mfululizo wa hali na mambo ya kukatisha tamaa lakini uamuizi wako wa kutokata tamaa kwa jambo lolote ndio uamuzi utakaokufanya kuwa mshindi kila wakati.