March 18, 2018

Mambo muhimu ya kufanya katika ndoa kama mwanaume.

1.Ndoa yetu haitakuwa na mfumo dume. Mimi na wewe tutakuwa na ndoa yenye mfumo wa demokrasia. Maamuzi ya ndoa yetu ni yale ambayo tumekubaliana kwa pamoja.

Nakuahidi kukushirikisha katika maamuzi yetu kiujumla. Maisha baada ya ndoa yetu yatakuwa katika maamuzi yetu sote na sio mimi peke yangu.

2.Utakuwa rafiki, mshauri wangu,mama wa watoto wangu na mwisho utakuwa mke wangu mpenzi. Kumbuka mwanaume wako ni mimi. Katu, usiongee na mwanaume mwingine kuhusu matatizo yako. Moyo wako ni wangu. Nishirikishe mimi. Nakuahidi kukusikiliza na kukujali kwa hali na mali na kuhakikisha unalo bega langu la kujiinamia.

3.Nitayabeba majukumu yangu ya kuwa mume wako na baba wa familia yako. Pesa yako itakuwa ziada tu pale nitakapokosa. Nakuahidi kufanya kazi kwa bidii kwa ajili ya yako na familia yetu.

4.Nakuahidi kukuchangamsha kihisia na kiakili. Nataka kuwa mwanaume ambaye sitabadilisha ule ubora uliokuwa nao, bali nitakuongezea thamani ya kuwa bora zaidi. Sitaogopa kukuonesha wazi hadharani ni kiasi gani nakupenda na kwa namna gani ulivyo wa thamani kwangu.

Nakuahidi kukutia moyo na kuwa pembeni yako katika kukusaidia kutimiza ndoto zako.

5.Kila mara nitajaribu kukutazama usoni mara kwa mara ili kukuhakikishia hisia za upendo wa dhati nilionao juu yako. Nakuahidi kukufuta jasho sio kwa kitambaa changu bali kwa mikono yangu mwenyewe.

6.Pamoja na kuwepo na vishawishi vingi vilivyopo mbele yetu. Nitajitahidi kukufanya uwe mwaminifu kwangu ili litawezekana ikiwa tu utajifunza uaminifu wangu nitakaokupatia kwako.

Nataka ujifunze kupitia mimi. Nakuahidi kuwa mkweli, muwazi na mwaminifu kwako. Nataka niwe bora kwako.

7. Kuna wakati nitakuwa na marafiki. Tutaenda na kupitia migahawa yote mizuri, nakuahidi kutoingia kununua chakula kama hakuna sababu hata kama nitakuwa na njaa ili tu nipate hamu ya kula chakula chako ulichoniandalia nyumbani.

8.Mke wangu hautokuwa mfanyakazi wangu, sitasubiri urudi nyumbani toka kazini uniandalie chakula. Kama nimewahi kurudi nyumbani nitaandaa chakula kwa ajiri yetu sote.
Kuna wakati nitataka ule chakula nilichokupikia mimi mumeo. Naahidi kufanya haya.

9.Nakuahidi kutotunza makosa yako kichwani mwangu.Nataka kukuona ukijiamini.Nitakuelezea ni namna gani ulivyo mzuri na sio kwa kuzungumza tu bali kukufanya uwe na amani na furaha, ili uzuri wako ujitokeze kila siku. Nitakusamehe ukiniomba msamaha wenye kumaanisha.

10. Sitaruhusu machozi yako yatiririke kwa ajili ya matendo yangu mabaya kwako. Wewe ni mwanamke bora kuliko wanawake wote niliopata kuwa nao. Unastahili kuwa na furaha, faraja, kupendwa na sio kuwa na huzuni kila muda, kukosa usingizi, na kulia lia.

Sio tu nataka kukufanya uwe peke yako. Pia nitakuwa mwanaume wako bora maishani. Huku nikijivunia kuwa nawe. Nitakuombea kwa Mungu nami niombee.

11.Nakuahidi kupigania moyo wako, kwa kuwa kiongozi mwenye huruma na hofu ya Mungu. Sitakuhukumu. Nitajaribu kuwa msikivu na kukufanya kuwa mwanamke bora. Nataka tuishi katika ndoto zako.Nakuahidi hili.

12.Nakuahidi kukupatia muda wangu kwa ajili yako. Nitakuwa pembeni yako kila utakaponihitaji. Nitakujali zaidi na sitakuacha utakapokuwa hoi kitandani kwa ugonjwa. Nitakuwa mbunifu wakati mwingi na wewe.Nitakusikiliza na kukupa moyo wakati utakapokuwa haupo vyema kimawazo.

13.Sitaacha kukuambia "NAKUPENDA" tena kwa kumaanisha kila wakati. Tutakapohudhuria tukio lolote lile sitakutambulisha kuwa wewe ni mama watoto wangu bali nitakutambulisha kuwa wewe ndiye mke wangu mpenzi na mwanamke nikupendaye. Hadharani nitajivunia.

14. Nakuahidi kukupatia uhuru wenye mipaka. Kukupatia vitu vizuri vyenye thamani vilivyo ndani ya uwezo wangu. Kipindi cha kuishi pamoja. Nitakuwa kiongozi wa ndoa yetu nawe utakuwa kiongozi wa nyumba yetu.

Wakati wote utakapofanya vyema nitakuonesha shukrani kwako kwa sababu nyumba ya mwanaume haiwezi kuwa bora bila mwanamke bora. Moyo wako ni hazina yangu.