March 30, 2018

Mambo ya kufanya ili uwe na tabia nzuri.

Hapana shaka karibu kila mtu angenijibu kuwa ana tabia nzuri. Wachache wangekuwa jasiri kiasi cha kukiri kuwa wana tabia mbaya hasa mbele ya mtu wasiyemfahamu kama mimi.
Lakini, pia siyo rahisi kwa mtu kukaa kando yake yeye mwenyewe akajitazama na kutambua kuwa ana tabia nzuri au mbaya. Kutokana na dhana hii na mazoea tulio wengi hatujui kama tabia zetu ni nzuri au mbaya.
Wako baadhi yetu waliobahatika kujua tabia zao zilizo mbaya na zile zilizo nzuri. Hata hivyo, kutokana na umuhimu wa mtu kuwa na tabia njema katika maisha haifai kulichukulia suala la kujitambua kama jambo la bahati.
Hatuna budi kufanya juhudi ili kujielewa sisi wenyewe kwani hali hiyo itayafanya maisha yetu na wale tunaoishi nao kuwa ya furaha.
Ninakumbuka kuna wakati niliwahi kuandika kuwa mtu huendelea kujifunza na kujenga tabia yake hadi mwisho wa uhai wake.
Wala hakuna mtu anayeweza kusema amechelewa kurekebisha au kuboresha tabia yake. Tena inabidi mtu aitambue yeye mwenyewe tabia yake mbaya kabla mtu mwingine yeyote hajagundua.
Ili tuweze kujenga au kuboresha tabia zetu inabidi kwanza tutambue jinsi tabia za binadamu zinavyojengeka.
Ujenzi wa tabia ya binadamu huanza tangu anapozaliwa. Wanasaikolojia huita ujenzi wa tabia ni mapambano baina ya haiba ya mtu na mazingira yake. Tangu mtu anapoanza kuzongwa na changamoto za maisha huanza mchakato wa kujifunza jinsi ya kukabiliana nazo.
Wote tunapokuwa wadogo huanza kujifunza jinsi ya kuendana na wazazi, kaka na dada zetu na hatimaye watu wengine nje ya kaya zetu. Tunapokuwa na kukomaa kiakili ndipo tunapojenga tabia au mwenendo unaofuata mfumo maalumu. Unapochunguza vitendo mbalimbali wanavyofanya watu waliopo karibu yako utagundua kuwa wanafuata utaratibu ambao huitwa “mchakato wa kujihami” Huu ni mchakato ambao mtu huutumia ili kuhakikisha usalama wake na kukidhi shauku na matakwa yake.
Tabia za kujihami huwa zinasababishwa na mawazo yako mwenyewe au kutokana na mambo mbalimbali yanayotokea ulimwenguni.

Kujengeka kwa tabia za binadamu

Mtu anapokua na akili yake kukomaa uwezo wa kujenga au kuboresha na hata kuzitupilia mbali baadhi ya tabia zake huwa mikononi mwake. Ataweza kufanya hivyo anapokuwa ameelewa vyema jinsi tabia ya binadamu inavyojengeka.
Ifuatayo ni mifumo mitatu ambayo husababisha kujengeka kwa tabia ya binadamu.

Kugeza

Namna moja inayompatia tabia au mwenendo fulani binadamu ni kugeza. Neno hili lina maana ya kuigiza, kufuata au kulinganisha. Kama tulivyoeleza mwanzo mtu anapopata akili na kujitambua hugundua kuwa kuna mambo ambayo ameiga kutoka kwa watu walio karibu naye yaani wazazi, walimu, ndugu na jamaa.
Baadhi ya mambo hayo ni kama vile nasiha, hisia, matakwa, elimu, maarifa, mwenendo wa kuchuzana na watu, mtindo wa kufanya kazi na pengine hata namna ya kuongea na ishara za kujieleza.
Vilevile, tunaweza kuigiza tabia hasi kama vile chuki, ukorofi, wivu, uhasama, usununi na mengineyo.
Hata hivyo, tafakuri na dhamira yetu huweza kutufanya tukazikana na kuziacha baadhi ya tabia tulizoiga au zile tulizofundishwa na wazazi au jamii baada ya kuziona hazifai na wala haziendani na haiba zetu. Ni lazima kuitazama kila tabia kwa pande mbili yaani wa manufaa na wa madhara yake.

Kujinasibisha

Namna nyingine ya kupata tabia au mwenendo fulani ni kwa kujinasibisha. Neno hili lina maana ya kujifananisha au kujishirikisha. Tunapokuwa katika kikundi kama vile cha kijamii, kiuchumi au kielimu huwa tunalazimika kuwa na mwenendo au tabia zitakazotufanya tufanane na kukubalika na wenzetu katika kikundi.
Kanuni ya kujinasibisha pia huendelea katika nyanja nyingine nyeti. Kwa mfano mtu anapoingia katika mapenzi, analazimika kwa kiwango fulani kufikiri na kutenda kama mpenzi wake ili wapatane na kwenda sambamba.
Kwa kawaida mtu mwenye akili timamu ni mwingizaji hodari hawezi kushindwa kujinasibisha kila inapobidi.

Kubadilisha kibaya kwa kizuri

Njia nyingine ya kujenga tabia ni kubadilisha mwenendo mbaya kwa mwenendo mzuri. Kwa kawaida binadamu huwa na misukumo ya kisaikolojia ya aina mbili. Aina moja ni misukumo chanya ambayo hujionyesha katika fikra na vitendo vya kujenga kama vile upendo, ukarimu, ucheshi, uadilifu na vitu vingine vya aina hii. Aina nyingine ni misukumo hasi inayoonekana katika mambo kama vile chuki, uhasama, wivu, choyo na vingine vya mfano huu.
Mtu anapotaka kuishi kwa furaha kufuata sheria mila na maadili ni lazima aichunguze misukumo ya kisaikolojia aliyonayo. Ikiwa ana misukumo hasi ni lazima azigeuze hisia na mawazo yake yawe katika mwelekeo mnyoofu kwa maana nyingine ni kuzitambua zile tabia au nyendo alizonazo ambazo hazikubaliki katika jamii na kuzibadili au kuziacha kando na kuzifuata tu zile zinazokubalika.
Mwishoni napenda kusisitiza kuwa katika hii mitindo mitatu ya kujenga tabia ule wa kubadilisha mabaya kuwa mazuri unaishinda yote kwa uzuri.
Mitindo ya kugeza au kujinasibisha wakati mwingine inaweza kutumika vibaya na kusababisha madhara hususan mtu anapoiga au kujinasibisha na watu wasio waadilifu.