March 27, 2018

Mwanaume ajifungua mtoto baada ya kupata mimba kutoka kwa mkewe.

Inafahamika dunia nzima kwamba wanawake ndiyo wanaobeba ujauzito, lakini je, umewahi kudhani kwamba inawezekana kwa mwanaume kubeba ujauzito kwa miezi tisa na kujifungua?

Vuta picha unakutana na watu wawili barabarani, mmoja amevaa mavazi ya kiume na hata mwonekano wake ni wa kiume na mwingine amevaa mavazi ya kike na hata mwonekano wake ni mwanamke kabisa, lakini mmoja kati yao ni mjamzito, unajua ni yupi kati yao? Ni yule aliyevaa mavazi ya kiume na mwenye mwonekano wa kiume!

Ni jambo lisilowezekana si ndiyo? Basi kwa taarifa yako, tukio kama hilo limetokea nchini Ecuador ambapo Fernando Machado, 22, amepewa ujauzito na ‘demu’ wake, Diane Rodriguez, 33.

Ilikuwaje? Diane Rodriguez alizaliwa akiwa mwanaume lakini mwenyewe akawa hajikubali kabisa, akawa anatamani kuwa mwanamke, jambo ambalo baadaye lilimfanya abadili jinsia na kuwa mwanamke. Hata hivyo, katika zoezi lake la kubadili jinsia, Diane anaeleza kwamba viungo vyake vya uzazi havikufanyiwa mabadiliko yoyote.

Kwa nje akawa na mwonekano wa kike kabisa, akawa na matiti kama wanawake wote walivyo, akajibadilisha kila kitu kuanzia mavazi, mitindo ya nywele, kutembea na kila kitu, maisha yakaendelea. Baadaye, akiwa ‘mwanamke’, Diane alikutana na Fernando Machado ambaye naye alikuwa akifanana naye baadhi ya vitu.

Tofauti yao ikawa ni kwamba Fernando alizaliwa akiwa mwanamke lakini akawa hapendi jinsia yake halisi.
Hali hiyo ilimfanya naye abadili jinsia na kuwa ‘mwanaume’ lakini kama ilivyokuwa kwa Diane, viungo vyake vya uzazi havikubadilishwa chochote zaidi ya mwonekano wa nje.

Wawili hao walikutana kwenye mitandao ya kijamii, wakajenga urafiki na baadaye wakawa wapenzi lakini mapenzi yao yalikuwa ya kustaajabisha sana kwa sababu yule ambaye kila mtu alikuwa akiamini kwamba ndiyo mwanaume, kiuhalisia alikuwa ni mwanamke. Na yule ambaye watu wa nje walikuwa wakimuona kama ndiyo demu, kiuhalisia ndiye aliyekuwa mwanaume.

Maisha yaliendelea na baadaye, Fernando ambaye sasa alikuwa na mwonekano wa kiume, akanasa ujauzito aliopewa na Diane ambaye ana mwonekano wa kike. Kwa hiyo ikawa ‘mwanamke’ amempa mimba ‘mwanaume’.

Septemba, 2016, Fernando alijifungua salama na sasa wanalea mtoto, huku wakieleza malengo yao kuwa ni kupata watoto wengi zaidi.