April 4, 2018

Historia fupi ya maisha na ustaa wa Nandy pamoja na kampuni yake.

KATIKA pasipoti yake ya kusafiria anatambulika kwa jina la Faustina Charles lakini kwa mashabiki wa Muziki wanamtambua kama Nandy a.k.a African Princess.

Ukiongelea miongoni mwa wasanii wa kike waliopo kwenye chati kwa sasa huwezi kumuacha. Ngoma iliyomtambulisha ilikuwa ni Nagusa Gusa ambayo remix yake amemshirikisha Mr.Blue. Haya ni baadhi tu ya mambo usiyoyajua kuhusiana na Nandy.

Nandy alikuwa moja kati ya washindi wa kwanza kabisa katika Shindano la Karaoke Barani Afrika la Tecno Own The Stage lililofanyika Februari 2016 nchini Nigeria.

Katika shindano hilo, aliibuka nafasi ya pili na kujizolea shilingi milioni 36 pia kuahidiwa kuingia katika lebo kubwa nchini Nigeria ya Chocolate City na kufanya kazi huko lakini alikataa na kujiunga na Jumba la Vipaji (THT) ambao yupo nao hadi sasa.

Nje ya muziki, Nandy ni bonge dizaina kwa mastaa…mavazi yake yote anayoonekana amevaa ya asili huwa anabuni mwenyewe na kushona. Miongoni mwa watu maarufu aliowahi kula shavu la kuwa-bunia baadhi ya mavazi hayo ni Naibu Spika Dk. Tulia Ackson.

Kati ya vitu anavyojivunia kupitia kipaji chake ni pale alipokuwa mshindi wa pili katika shindano hilo la Karaoke na kujipatia shilingi milioni 36 ambazo nusu yake zilimuwezesha kumiliki kampuni yake mwenyewe ya kubuni na kutengeneza mavazi ya asili na magauni ya harusi iitwayo Nandy African Print.

Kipaji chake kilikuwa kitoke kwa mara ya kwanza Akili Records chini ya Akili The Brain. Nandy anasema kuwa katika kuhangaika kwake kutoka kimuziki alishawahi kufika kwenye studio yake na kutengeneza ngoma nne lakini hazikufanikiwa kutoka mpaka alipopata shavu la kwenda Nigeria kwenye Karaoke ya Tecno.

Source: Global Publishers.