April 26, 2018

Anza na ulichonacho kupata mafanikio.


Kisaikolojia na kimaumbile binadamu wote ni sawa ila tunatofautiana jinsia na matumizi ya vitu tulivyopewa na mwenyezi Mungu. Na hii ndio hupelekea tofauti kubwa kati ya walichonacho (Matajiri) na wasionacho (maskini). 

Ili kufanikiwa haijalishi upo katika hali gani, kitu kikubwa kwako "Anza Na Ulichonacho Kupata Mafanikio". Unaweza ukajiuliza kivipi? Usipate tabu. Ungana nami nikuhabarishe na kukupa nyundo za kukuzindua katika usingizi ili upate mafanikio ya kweli.

1. Akili. 
Ni ukweli kwamba kila binadamu ana akili ya kung'amua jema na baya ila sio wote wanaojua thamani ya akili walizonazo. Wapo wanazitumia kwa faida na malengo na kupata mafanikio ila wapo wanaozitumia vibaya na kuishia kuishi maisha shida hadi wanakufa. Katika kuitumia akili ndipo huonekana tofauti ya wanaojua na wasiojua kitu. 

Wanaofuata mkumbo na wanatumia akili zao kufikiri na kuamua ni nini wafanye, kivipi na wakati gani. Ili kuonyesha matumizi sahihi ya akili kila binadamu anatakiwa kufikiri na kuwaza kabla ya kuamua kufanya jambo lolote katika maisha yake. 

Ni vyema tusiwe watu wa kuamini kirahisi tunayoona na kusikia kwa watu na kuyafanya bila tafakari. Tuzitumie akili zetu katika kujituma na kufikiri kwa utofauti na wanavyofiki wengine . Tuwe tayari kujifunza kwa wenye elimu juu ya kile tunataka kufanya na sio kuiga wanavyofanya watu wengine. 

2. Muda. 
Kila binadamu awaye ana muda na amepewa muda wa kuishi na kufanya mambo yake kwa uhuru na amani . Lakini si watu wote wanaoutumia muda wao vizuri katika kujipatia mafanikio. 

Wengi hutumia ujana wao katika starehe, ulevi na kujirusha. Wengine wanatumia muda wao katika kufuatilia maisha ya watu umbea na majivuno. Pamoja na kutumia muda hovyo lakini kumbuka, huo ndio muda wako wa kujitafutia maisha na mafanikio. Muda ndio rasilimali muhimu kuliko zote ukiutumia vizuri hakika mafanikio utafanikiwa. 

Embu jiulize kuna tofauti gani kati ya tajiri na masikini katika muda? Kila mtu ana masaa 24 tofauti ni matumizi tu . Ukafatilia utagundua, tajiri ana panga malengo na mipangilio yake katika siku wakati maskini hana mipangilio na muda wake anaweza kushinda asubuhi hadi jioni anaangalia Televisheni au movie ambazo hazimsaidii kitu katika maisha yake. Jiangalie vizuri unatumiaje muda wako ili kuyafikia mafanikio yako?  

3. Watu. 
Kila mtu iwe kwa kutaka au kutotaka amezungukwa na jamii ya watu. Na kimsingi umepewa watu hao na Mungu ili uweze kuwatumia na kupata kile unachotaka. Kuna wale wa hiyari na ambao unalazimika kuwatafuta mwenyewe ili wakusaidie kupata kile unataka katika maisha yako. 

Kwa mfano mwalimu inabidi umtafute ili akupe elimu, wataalamu wa afya inakulazimu uwafuate ili wakutibu. Lakini kuna watu ambao umepewa bila kutaka au kupanga wewe kama wazazi, ndugu, wajomba na mashangazi. 

Hakuna aliyepanga kuzaliwa na wazazi fulani au kuzaliwa tumbo moja na mtu fulani bila kujali ni masikini au tajiri. Lakini kutokana na watu hawa unaweza na unapaswa uwatumie katika ushauri na maarifa waliyonayo ili kupata kile unachotaka ambacho si kingine ni mafanikio. Kushindwa kwako kuwatumia watu hawa hili litakuwa ni tatizo lingine ambapo ukishindwa kufanikiwa usimlaumu mtu. 

4. Kipawa / kipaji. 
Huu ni uwezo wa ndani alionao kila binadamu bila kujali kabila lake au rangi yake ana kile anachoweza kukifanya tofauti na wenzake. Hicho ndicho kipaji na mtu akikigundua na kukitumia vizuri hupata mafanikio kwa haraka.

Tena ndio wale ambao muda mfupi hupata utajiri wa ghafla na watu kusema kajiunga na Freemason huyo au amemuua mama yake ili apate utajiri na maneno mengineyo. 

Siku zote tafuta ukijue kipaji chako na kitumie upate utajiri na mafanikio katika maisha yako. Unapokuwa na kipaji na ukikitumia ipasavyo mafanikio makubwa yanakuwa upande wako. 

Jaribu kuangalia watu wote ambao walimudu kutumia vipaji vyao kwa namna moja au nyingine maisha yao yako vipi, bila shaka ni ya mafanikio makubwa sana. 

5. Nguvu. 
Kila mtu amepewa nguvu na uwezo wa kufanya jambo fulani.Tunaweza kuzitumia nguvu zetu katika kilimo, biashara na hata kazi yeyote halali na kujipatie kile tunataka katika maisha.

Tatizo watu wengi tumebweteka tunataka maisha simple/rahisi tulale tuamke kesho matajiri bila kufanya kazi. Vijana wengi utakuta wanataka kufanya kazi rahisi na kupata faida kubwa. 

Wanacheza mchezo wa kubeti wakiamini watatoka kimaisha, wanacheza bahati nasibu wakiamini watapata utajiri, wengine wanauza miili yao wakiamini ndio njia pekee ya kupata maisha mazuri na bora kumbe wanapotea na kuharibikiwa kabisa. 

6. Afya. 
Kila binadamu amepewa afya ya mwili kabla ya kufikwa na maradhi. Tunapaswa tujue uzima na afya ni majaaliwa ya mwenyezi Mungu hivyo tuzitumie vizuri afya zetu katika kupata kile tunataka katika maisha yetu. 

Afya ni kitu cha muhimu kukilinda na kukitumia vilivyo kwa faida ya maisha yetu. Ili tufurahie maisha yetu lazima tujali afya zetu kwa kula vyakula bora na vinywaji bora. Na sio kula ilimradi chakula. Na kunywa ilimradi tu au kwa kuwa watu wanakula nasi tule. 

Tujitahidi kuzilinda na kuzitumia vizuri afya zetu ili tuweze kutimiza malengo yetu tuliyojipangia katika maisha. Bila afya nzuri hakuna Mafanikio. Kila mtu na azingatie mbinu hizi katika mafanikio yake zitamsaidia na kumwongoza.