April 26, 2018

Mambo 10 ya kujikumbusha katika safari ya mafanikio kila wakati.

Safari ya mafanikio ina mambo mengi ambayo unatakiwa uyajue na kuyafanyia kazi kila siku. Na unapoyafata mambo hayo ndio unazidi kujitengenezea msingi mkubwa wa kufanikiwa kwako kwa kile unachokifanya.

Leo katika makala haya nakukumbusha baadhi ya mambo ya msingi ya wewe kuyakumbuka kwenye safari yako ya mafanikio. Haya ni mambo ya msingi kwa sababu, ukiyatumia yatakutoa kutoka kwenye hatua moja na kukupeleka hatua nyingine.

1. Unapowasaidia watu, ujue hiyo ni  sawa na kujisaidia wewe mwenyewe. Itafika wakati ule msaada unaoutoa kwa ajili ya watu wengine nao msaada huo utakurudia wewe kwa namna ya tofauti ambayo hujaijua bado.

2. Hakuna matokeo ya papo kwa papo ambayo unaweza kuyapata kwa chochote kile unachokifanya kwenye maisha yako. Unachotakiwa kufanya ni kuweka juhudi na kusubiri. Mafanikio ni matokeo ya kuwekeza juhudi na kuweza kusubiri. Kama hutaki kusubiri sahau kupata mafanikio yoyote makubwa maishani.


3. Ni muhimu kuboresha afya, ni muhimu kuboresha kipato, ni muhimu kuboresha mahusiano sahihi na wengine na muhimu pia kuwa na maarifa bora na sahihi. Unapokuwa unaboresha mambo hayo kila siku unajitengenezea uhakika mkubwa wa kuyafanya maisha yako kuwa bora sana karibu kila siku.

4. Kama kuna kitu unakihitaji kweli na kwa moyo wote, ni kweli lazima kitu hicho hata iweje ni lazima utaweza kukipata, Hautaweza kuweka sababu wala hutaweza kutoa visingizio kivile. Utakachokifanya ni kufanya kila linalowezekana mpaka kitu hicho uweze kukipata. Ni kipi ambacho unakitaka, usiweke sababu, kitu hicho utakipata.

5. Moja ya kitu ambacho unatakiwa kukisahau kabisa ni juu ya umri wako na kuendelea kuishi. Umri wako usikuzuie kufanya kitu chochote, bali wewe kama ni kuwekeza endelea kuwekeza sahau habari ya kwamba sasa hivi umri wako ni mkubwa. Kama unababaishwa na umri utapotea na maisha yanaendelea kusonga mbele.

6. Maisha ya kufanya makosa ni bora zaidi kuliko kuishi maisha ambayo hufanyi makosa kabisa. Ni bora uishi kwa kufanya makosa kabisa na hiyo itakusaidia kufika mbali kuliko ukae tu hufanyi kitu kisa eti unaogopa kukosea.

7. Mara nyingi kwenye maisha hatuoni vitu kama vilivyo kwa uhalisia wake, bali tunaona vitu kama tunavyoviona sisi kwa mitazamo yetu na sio kinyume cha hapo.

8. Hamna kitu cha maana kuwa nacho kama amani moyoni mwako. Unapokuwa na amani moyoni hiyo ndiyo inayokupa nguvu ya kufanya mambo makubwa kwa jinsi unavyotaka wewe. Anza leo kutengeneza amani moyoni ili ikupe faida kubwa kwako.

9. Unaweza kufurahia maisha yako popote na wakati wowote pasipo kujali mtu, kitu au hali ya aina fulani. Ni kitendo cha kuamua kuyafurahia maisha yako tu, na ukishaamua kuyafurahia maisha yako na kweli utayafurahia hayo maisha.

10. Kama unaweka nguvu za uzingativu, juhudi na mabadiliko chanya kwenye kila hatua unayofanya, hata kama huoni mabadiliko ya wazi, tambua kabisa, wakati utafika maisha yako yatabadilika kabisa.