April 1, 2018

Mambo ya muhimu kuyaweka kuwa siri maishani mwako.

Siri si kitu kibaya, na kutunza siri ni uwezo ambao kila mmoja wetu anapaswa kujifunza kuwa nao. Kwa bahati mbaya, utunzaji wa siri ni jambo ambalo limewapita kushoto watu wengi kiasi cha kuwasababishia matatizo watu wanaoyafungukia masikio yao.
Kutokana na udhaifu huo je, ni mambo gani hayo ambayo yanapaswa kuhifadhiwa kwa siri?
Ndoto na Malengo Yako.
Usithubutu kuzishirikisha ndoto zako kwa kila unaye kutana naye, lah sivyo utaishia kukatishwa tama na ndoto zako zitafifia. Tafiti za saikolojia zinatueleza kuwa ukimshirikisha mtu ndoto na malengo yako kunakuwa na uwezekano mkubwa wa kushindwa kuzitimiza kwasababu hali hiyo itakusababishia kupoteza motisha ya utekelezaji.
Mshirikishe ndoto zako mtu anayeweza kukuelewa atakayeweza kukusukuma kwa kukutia moyo, mtu ambaye ana ujuzi wa kutosha na mambo unayoyahangaikia.
Kumbuka nukuu isemayo “Si kila mtu atakayeilewa safari yako. Na hiyo ni sawa! Uko hapa kuishi maisha yako, sio kufanya kila mtu akuelewe.”
Pia kumbuka nukuu nyingine isemayo “Muda wako ni wa thamani sana kiasi cha kutoruhusu kutenguliwa na watu hasi. Usimruhusu mtu yeyote akutenganishe na ndoto zako. “
Siri za Watu.
Mtu anapokwambia siri zake, ziache zibaki kuwa siri. Si busara hata kidogo kumwaga siri za watu hadharani, hasa kama ulisisitizwa kabisa kwamba mambo hayo ni siri. Ungejisikiaje kama siri zako zingewekwa hadharani na hatimaye uanze kunyoshewa vidole kila kona ya mtaa unayopita! Huo ubaya wa kuvujishiwa siri zako unaoweza kuusikia ndani ya moyo wako ndivyo vilevile anavyoweza kujisikia ndugu, mpenzi, rafiki, jamaa au jirani yako.
Mtu anapofikia hatua ya kukuambia siri zake maana yake anakuamini kuliko wengine, usimfanye ajutie imani yake, hata tumaini lake libatilike juu yako.
Pia unapoaminika na watu kiasi cha kuambiwa siri zao ni ishara ya heshima, usitake ipotee kwa sababu zisizo za msingi.
Historia mbaya ya mtu fulani.
Ikitokea umebahatika kuijua histori mbaya ya mtu Fulani, achana nayo. Hakuna haja ya kumdhihaki mbele za watu au kufichua mambo ambayo yamekwisha zikwa na mtu siku za nyuma. Kuna haja gani ya mambo ya kale ya mtu aliyekwisha kugeuza mwenendo wake? Hebu chukua dakika ukumbuke jambo baya ulilowahi kulifanya miaka mingi iliyopita kisha utafakari utajisikiaje ikiwa utakutana na mtu analiibua mbele za watu wakati ulishaachana kabisa na mambo kama hayo hayo!
Epuka kuibua siri za mambo mabaya ya kale kwa mtu anayejitahidi kubadilika, huko si kumsaidia mtu bali ni kumdhoofisha na kumkatisha tama kabisa.
Wajibu wako ni kuwatia moyo watu wanaofanya jitihada za kuachana na mabaya yao ya kale na si vinginevyo.
Siri za familia yako.
Si  jambo la busara kabisa kumwaga siri za familia yako hadharani. Tena ni jambo la aibu na la kusikitisha kuifanya familia yako kuwa kichwa cha mjadala mbele za watu. Ukizingatia wewe mwenyewe bado utaendelea kuwa mmoja wa familia hiyo na mwisho wa siku hao hao watu unaowamwagia siri chafu za familia yako watakugeuka na kuzitumia kukuangamiza mwenyewe. Tumia busara!
Kutoa siri za familia yako hakuiaibishi familia yako tu bali unajifungia milango ya msaada pia kwako wewe binafsi na pili kwa wanafamilia wenzako. Kutoa kwako siri hakukutenganishi na familia kwakuwa hakuana jambo liwezalo kuvunja undugu badala yake na wewe pia unahesabiwa kuwa mmoja wao.
Udhaifu wa Mpenzi Wako.
Hivi unapoamua kutoa siri za mpenzi wako unatarajia dunia ikuchukuliaje? Unakumbuka kwamba mke au mume ni sehemu ya mwili wako na yeye ndiye msiri wako wa kwanza kwasababu ndiye mtu pekee uliyemwamini kiasi cha kumruhusu kuujua hata utupu wako, sasa unapotueleza mapungufu yake unatarajia nini? Haujui kuwa unawapa watu siraha wanayoweza kuitumia kukuangamiza mwenyewe!

Mapungufu au Udhaifu wa mpenzi wako ni jukumu lenu binafsi, wewe na muhusika na hata mnaposhindwa kufikia muafaka wa makubaliano juu ya jambo linalowatatiza ni busara kumshirikisha mtu anayejitambua na mwenye busara ya kuweza kuwatunzia siri zenu na sio kupayuka mapungufu yake hadharani.
Heshima, upendo, busara, hekima na chochote kizuri, vinaanzia kwako mwenyewe, kama haujiheshimu, haumheshimu mpenzi wako ambaye ni mtu wako wa karibu usitegemee kulipwa fadhira na dunia. Tumia busara!!!
Kutunza siri ni wajibu wa kila mmoja wetu, hata kama unajisikia msukumo kiasi gani, usitoe siri za watu!
Utachukua hatua gani ukimshuhudia mtu akitoa siri za rafiki, ndugu au mpenzi wako?Utachukua hatua gani ukigundua kuwa mpenzi wako anatangaza udhaifu wako wa faragha nje?