April 3, 2018

Mambo Yanayo Boresha Afya Ya Msichana


Chakula bora na mlo kamili

Wasichana wanahitaji mlo kamili na chakula kingi zaidi ya wanawake watu wazima wenye uzito sawa na wao. Katika kipindi hiki cha makuzi na kupevuka msichana huhitaji viini lishe vya kutosha. Katika kipindi hiki protein, madini ya chokaa, chuma na zinc huhitajika mara dufu. Vitamini, wanga na mafuta pia huhitajika kwa wingi.

Kupoteza damu wakati wa hedhi na mchakato wa kukua huongeza mahitaji ya madini chuma katika mwili wa msichana. Msichana anahitaji kula chakula chenye asili ya mimea, kula matunda na maji ya matunda (juice) kwa wingi. Nafaka na mboga za majani, vyakula vitokanavyo na mizizi kama karoti, viazi na vyakula vingine ni muhimu sana.

Wasichana inawapasa kuepuka vyakula visivyo na viini lishe vya kutosha, vyenye sukari nyingi, chumvi nyingi pamoja na mafuta mengi ambavyo huandaliwa kwa harakaharaka au kufungashwa viwandani (junk foods). Vyakula vya namna hii, vinaweza kusababisha matatizo ya kiafya kama vile kutoa kinyesi kikavu, unene wa kupindukia, kisukari, shinikozo la damu, uchovu wa mwili wa mara kwa mara, uvimbe wa maungio na vifundo vya mwili pamoja na magonjwa ya figo.

Ni muhimu pia kuepuka ulaji wa kiasi kikubwa cha nyama na mafuta na kuepuka vinywaji vyenye caffein kama vile majani ya chai, redbull, cocoa, chocolate na baadhi ya soda. Vinywaji vyenye coffein husababisha madini ya chuma yasifyonze au kusharabiwa na mwili kutoka katika chakula tunachotumia kwa kiwango kinachotosheleza. Vinywaji hivi pia huongeza kasi ya kupotea kwa madini ya chokaa kwa njia ya mkojo.

Kuhusiana na habari ya lishe bora vilevile, ni busara msichana kuepuka matumizi ya pombe. Upo uhusiano kati ya matumizi ya pombe na saratani ya matiti pamoja na magonjwa mengine ya mwili wa binadamu. Kula chakula bora huleta maana pale tu chakula hicho kinapoliwa kwa namna inayofaa. Usile chakula kama huna njaa au kama umeshiba. Usile chakula kingi wakati wa usiku, chakula kiliwe taratibu bila haraka na kitafunwe sawasawa kabla ya kumeza.

Kudhibiti uzito na unene wa mwili

Kunenepeana kupita kiasi kwa msichana kunapunguza afya, uzuri na urembo wa msichana. Kimsingi unene ni matokeo ya mtindo wa maisha, kula chakula kingi kuliko kinavyotumika mwilini kutokana na kazi alizonazo mhusika au maumbile ya kijenetiki na vinasaba. Ili kukabiliana na tatizo hili msichana hana budi kupunguza vyakula vyenye mafuta, chumvi na wanga kwa wingi. Pia hana budi kufanya kazi kwa bidii na kufanya mazoezi ya mwili kila siku, jambo hili husaidia sana katika swala la kudhibiti unene. Kwa ajili ya afya inashauriwa kufanya mazoezi kwa dakika 30 hadi dakika 40 kila siku.

Zipo faida nyingi kwa msichana anapodhibiti unene wa mwili wake. Msichana mwenye uzito wa wastani anakuwa na afya nzuri ya ngozi, misuli na mifupa. Anapata afya njema kihisia na kudhibiti msongo, hali hii humsaidia kupata usingizi mzuri, kutengeneza umbo zuri la kike, ukakamavu na huleta mwonekano wa ujana zaidi.Wasichana wanaofanya mazoezi na kudhibiti unene wanapunguza pia uwezekano wa kupata uvimbe katika mji wa uzazi na katika mifuko ya mayai.

Kutumia maji kwa wingi

Inakadiliwa kuwa kati ya asilimia 45-75 ya mwili wa binadamu ni maji. Kila chembechembe hai ya mwili wa binadamu inahitaji maji ili iweze kufanya kazi zake sawasawa. Damu ina maji takribani asilimia 80, na asilimia 50-70 za misuli ni maji, mifupa inakadiliwa kuwa na maji kati ya asilimia 20-33 hivi.Ni hakika kuwa mwili wa binadamu utashindwa kufanya kazi zake vema kama utapungukiwa maji. Usagaji wa chakula tumboni, uondoaji wa taka mwilini kupitia mkojo, jasho na kinyesi pamoja na urekebeshaji wa joto la mwili vyote hivi vinahitaji maji ya kutosha hasa yale ya kunywa.

Zipo sababu nyingi zinazochangia mwili kuhitaji maji kwa wingi. Mtu anayeishi katika maeneo yenye joto jingi, anayefanya mazoezi au mtu mgonjwa mwenye homa kali, anahitaji maji kwa wingi kuliko kawaida. Vilevile matumizi ya chakula chenye chumvi nyingi, sukari na proteni kwa wingi hongeza hitaji la maji mengi mwilini. Mambo mengine yanayochangia ongezeko la hitaji la maji mengi mwilini ni pamoja na kutapika, kuharisha na ugonjwa wa mafua kutokana na upoteaji wa maji mengi toka mwilini.

Maji mengi ya kunywa huboresha afya ya msichana kutokana na kuimarisha utendaiji wa figo, ubongo, moyo na kibofu cha mkojo. Maji pia husaidia kuondoa sumu ndani ya mwili kwa urahisi na kulainisha ngozi ya msichana na kumfanya aonekane mrembo na mwenye afya kamili.Msichana akipungukiwa na maji mwilini hupata kiu ya maji, huwa mchovumchovu, ngozi yake hupoteza uwezo wake wa kuvutia, hupata mkojo kidogo na mwekundu unao ambatana na maumivu wakati wa kukojoa. Hushindwa kupata choo/ haja kubwa vizuri, hupata homa na wakati mwingine msukumo wa damu mwilini hushuka na kupata maumivu ya kichwa.

Ili kuwa na afya njema msichana anashauriwa kunywa maji si chini ya lita 2.5 kila siku. Ni vizuri kunywa maji zaidi ya dakika 15 kabla ya chakula na dakika 30 baada ya kula chakula ili kutoa nafasi kwa tumbo liweze kusaga chakula vizuri. Kunywa maji wakati wa kula chakula, huzimua dawa za tumbo zinazofanya kazi ya kusaga chakula. Hali huwa mbaya zaidi hasa maji hayo yanapokuwa ya baridi sana. Maji baridi husababisha tumbo kusimamisha kazi yake ya usagaji wa chakula kwa muda. Maji baridi pia hukata kiu haraka na kusababisha mtu asinywe maji ya kutosha. Kunywa maji ya uvuguvugu kidogo ni vizuri kwani yanaweza kuwa dawa ya maumivu ya mwili na kuimarisha afya ya njia ya hewa.

Ingawa maji yanahitajika zaidi ndani ya mwili kwa ajili ya kunywa, lakini pia tunahitaji maji juu ya mwili. Tunahitaji maji ya kuoga na kunawa uso au kunawa mikono kabla na baada ya kula chakula. Nje ya mwili wa binadamu ngozi huchafuka kwa jasho, vumbi na ngozi inayokufa kila siku ili kupisha chembechembe mpya za ngozi zinazozalishwa hasa wakati wa usingizi. Maji yanaweza kutumiwa kama dawa ya kukanda na kupunguza maumivu ya misuli na uvimbe wa viungo vya mwili. Maji ya uvuguvugu pia husaidia kupunguza maumivu ya kichwa kinachotokana na kukakamaa kwa misuli ya kichwa kwa sababu ya msongo.

Maji ya kuoga pia huchangamsha neva, huondoa bakteria wanaosababisha harufu mbaya ya mwili na huleta burudiko la mwili. Maji ya kuoga ni vema yakiendana na hali ya hewa, kama majira ya mwaka ni wakati wa baridi basi ni busara kuoga maji ya uvuguvugu na kama ni wakati wa joto ni vizuri kuoga maji ya baridi kiasi. Usafi wa ngozi kwa kutumia maji na sabuni husaidia vinyweleo vya mwili kutenda kazi zake vizuri na kukinga mwili dhidi ya magonjwa ya ngozi, kuharisha na minyoo.

Mapumziko na usingizi

Baada ya kazi ngumu ya mwili na akili, ni muhimu kupata muda wa kupumzika kila siku. Kupata usingizi wa kutosha na kulala mapema pia ni muhimu kwa afya. Kulala angalau kwa saa nane usiku na kupata angalau siku moja katika juma kwa ajili ya mapumziko makubwa huimarisha afya kwa namna ya ajabu kabisa. Mapumziko ni dawa ya kurejesha afya na nguvu za mwili zinazopotea baada ya kazi. Wakati wa mapumziko mwili unazalisha dawa zinazoponya majeraha yanayoletwa na masumbufu ya maisha pamoja na msongo. Msongo ni sehemu ya maisha ya kila siku hivyo basi ili kukabiliana na msongo ni lazima kupata nafasi na fursa ya kupumzika. Kukosa mapumziko na usingizi wa kutosha kunaweza kudhuru vibaya sana hali ya kinga mwilini na kasabisha magonjwa.

Kupata fursa ya kicheko

Kicheko ni muhimu kwa urembo na afya ya msichana, msichana anatakiwa kucheka kadri awezavyo hata kama kicheko ni cha kujilazimisha. Kicheko kina faida sawa na mazoezi katika kuimarisha afya ya misuli ya matama na tumbo.Tabasamu la mara kwa mara hufanya umbo la uso kuwa zuri na kupunguza makunyanzi ya uso. Kicheko pia husaidia mwilini kuzalisha kichocheo aina ya endorphin ambacho hufanya mwili kupata raha na hisia bora. Kicheko pia huimarisha kinga ya mwili, hupunguza msongo wa mawazo na husaida moyo kufanya kazi zake vizuri.

Kama unafikiri kwamba kicheko hakina faida basi nuna kwa mwaka mzima uone matokeo yake, lakini kama unafikiri kucheka kunafanya mtu ajisikie vizuri basi cheka sana ili ujisikie vizuri. Msichana anapotafuta afya kwa njia ya kicheko imempasa kuwa na kiasi, yaani kutenda jambo jema kwa wastani.

Kusikiliza muziki bora

Kupitia mfumo wa fahamu na hisia, muziki bora husafirishwa na kufika kila sehemu ya mwili na kuzalisha furaha, raha na msisimko wa mwili. Hali hii hutokana na uwezo wa muziki wa kuchochea mwili ili uzalishe kichocheo aina ya serotonin. Muziki ni muhimu katika uboreshaji wa afya ya msichana kwa vile hupunguza msongo wa mawazo, huondoa wasiwasi na kutibu sononeko la moyo. Muziki huondoa maumivu na kushusha shinikizo la msukumo wa damu.

Muziki hupunguza hali ya kukakamaa kwa misuli, huleta usingizi mzuri, huongeza uwezo wa ubongo kufanya kazi zake vizuri na kupunguza kasi ya kuzeeka. Muziki husaidia mwili kuzalisha vichocheo vya ukuaji wa mwili. Pamoja na faida zote hizo za muziki, ni bora ikumbukwe kuwa kusikiliza muziki wenye makelele na maneno yasiyofaa hudhuru afya ya mwili na akili pia.

Kuepuka kutazama mambo yasiyofaa

Kila tunachotazama, kusoma au kusikiliza kina mchango wa kuathiri maisha yetu kwa wema au kwa ubaya. Picha, mikanda ya video, vipindi vya luninga (television), mitandao ya kijamii au magazeti yasiyofaa yenye habari na picha zinazoendekeza ngono na ujambazi pamoja na mauaji, vinadhuru afya ya akili na mwili pia. Ni muhimu kuwa na mazoea ya kusoma mambo mema na kuepuka kutazama mambo yasiyofaa [1]. Kwa kufanya hivi unajizoeza kuwa na tabia pamoja na mazoea yatakayodumisha afya njema katika maisha yako ya sasa na baadae.

Kumbuka kuwa tabia njema unayoijenga sasa ndiyo itakayokuwa msingi wa maendeleo na mafanikio katika maisha yako ya baadaye. Na tabia mbaya unayoizoea sasa ndiyo itakayokuwa kikwazo kwa maendeleo, mafanikio na ndoto zako za maisha ya baadaye. Tabia zetu zina nguvu ya kuamua mstakabali wa maisha yetu kuliko tunavyofikiria.

Kuzingatia usafi

Afya ya msichana inategemea kwa kiwango kikubwa jinsi anavyozingatia usafi wake wa mwili na mazingira kwa ujumla. Usafi ndio kitovu cha afya, ustawi pamoja na urembo wa msichana.Usafi ni kinga madhubuti dhidi ya magonjwa mengi ya kuambukiza yanayoshambulia ndani ya mwili na nje ya mwili na kuharibu afya ya ngozi, kucha na nywele za msichana.

Kujihusisha na mambo ya ibada

Ibada husaidia mwili kudhibiti vichocheo vinavyosababisha ongezeko la shinikizo la msukumo wa damu mwilini. Ibada pia husaidia katika uzalishaji wa kinga ya mwili na kudhibiti unyongonyevu unaotokana na kukata tamaa. Ibada ya kweli husaidia wasichana kupata hisia za usalama na kupata maburudisho salama yanayorejesha afya ya kihisia na kuwaumba upya (recreations).

Tafiti mbalimbali za kisayansi zinaonyesha kuwa, watu wanaofanya ibada mara kwa mara wana uwezekano wa kuishi maisha marefu zaidi ikilinganishwa na wenzao wasiofanya ibada. Ibada ni dawa nzuri dhidi ya magonjwa mengi ya moyo na kinga dhidi ya aina nyingi za saratani.

Kufanya uchaguzi mzuri

Upo wakati ambapo msichana anakabiliwa na ulazima wa kufanya uchaguzi. Msichana anaweza kufanya uchaguzi wa mambo mengi kama vile mtindo wa maisha, mtindo wa kutunza nywele zake, uchaguzi wa dini, rangi ya nguo, uchaguzi wa marafiki, shule, mwenzi wa maisha (mchumba), chakula, vipodozi na kadhalika.

Kuchagua ni kufanya uamuzi wa kupendelea au kuteua kitu kimoja kati ya vitu vingi, uchaguzi pia unaweza kuwa juu ya mtu, jambo au tendo. Kufanya uchaguzi wakati mwingine ni jambo gumu hasa pale unapotakiwa kufanya uchaguzi mzuri na sahihi. Ili msichana awe na afya njema na kuidumisha, anakabiliwa na swala la kufanya uchaguzi. Ni lazima kuchagua kuwa na afya njema na kwa sababu hiyo, kuna mambo ambayo ni lazima kuyazingatia kila unapochaguwa kuwa na afya njema au urembo ulio salama.

Uchaguzi lazima uwe unaodumisha afya yako binafsi, afya ya wengine na afya ya mazingira.Uchaguzi lazima uwe salama na unaozingatia matakwa ya sheria na kanuni za maadili.Uchaguzi lazima uoneshe kuwa unajijali na kujali wengine pia.

Unapochagua mambo vilevile ni muhimu kukumbuka kuwa maisha yanabadilika kulingana na umri unavyobadilika au majukumu yanavyobadilika. Leo unaweza kuona kuwa mapambo ya kujichora mwilini kwa tattoo ni uchaguzi mzuri, lakini baada ya miaka kumi ukawa huna haja ya michoro hiyo. Hivyo basi ni vema tattoo hizo zisiwe za kudumu endapo utachagua kujipamba kwa namna hiyo.

Kuheshimu wazazi na watu wa makamo

Ili msichana awe na afya nzuri ya mwili, akili, roho na afya ya kijamii, hana budi kuwaheshimu wazazi wake na watu wa makamo katika jamii yake. Kuheshimu wazazi ni kutambua madaraka, majukumu, haki, wajibu na umuhimu wao kwa ajili ya mafanikio na ustawi wako katika nyanja mbalimbali za maisha.

Vijana wengi wanapofikia umri wa balehe, huwa na shida ya kuwa na mahusiano mazuri na ya heshima kati yao na wazazi wao au watu wengine wa makamo katika jamii. Hii inaweza kusababishwa na hali ya kukua kiakili, ambayo inamfanya msichana kutaka kuwa na maamuzi yake na kutumia nguvu za kufikiri bila kujali athari zake katika mahusiano.

Tatizo kubwa la vijana wengi huanza pale wanapojiona kuwa wamekuwa na kuona kuwa kila wanachofikiri ni sahihi. Na kwa sababu hiyo huanza kushindana na wazazi. Wazazi wanaposimamia maadili na ustawi na vijana wanaokabiliwa na hatari ziambatanazo na mabadiliko ya makuzi, vijana hushindwa kuelewa mambo hayo kutokana na ukweli wa kisayansi kuwa akili zao hazijakomaa, bado zinakuwa. Vijana hujitahidi kutatua matatizo ya kiutu-uzima kwa kutumia uzoefu wa kitoto na kufikiri kuwa wazazi wamepitwa na wakati.

Wazazi hawapitwi na wakati kama vijana wengi wanavyodhani, ukweli wa mambo ni kuwa wazazi wameona wakati uliopita na wanaona wakati uliopo. Vijana ambao hawakupata bahati ya kuuona siku za zamani ndio wanaostahili kujitambua kuwa wamepitwa na wakati wa zamani.Waswahili wanasema kuwa kuishi kwingi ni kuona mengi, na kwa hakika hakuna mwalimu mzuri katika maisha kama uzoefu. Elimu yoyote bila uzoefu ni elimu nusu, na hii ndiyo sababu waajili wengi wanapotafuta wafanyakazi wapya, wanauliza kuhusu uzoefu wa kazi.

Mungu ambaye ni mzazi na mzee wa siku nyingi asiyepitwa na wakati, anatambua kuwa wazazi hawapitwi na wakati. Muumba wetu anatusisitiza kuwaheshimu wazazi wetu, agizo la Mungu kwa wasichana na wavulana ni kutii na kuheshimu wazazi wa kibaiolojia na wale wa kambo hata kama ni maskini au wazee sana. Kuheshimu wazazi husaidia vijana kuwa na afya njema na maisha marefu.

Mungu amewapa wazazi jukumu la kuwafundisha na kuwatunza vijana ili wawe na afya njema kimwili, kiakili na kijamii. Anawaagiza wazazi wafundishe vijana wao mambo yale walioyaona zamani na kupata uzoefu wake kabla watoto hawajazaliwa, na hii ndiyo elimu iliyo bora.

Mahusiano mazuri kati ya wasichana na wazazi au watu wengine, huusisha zaidi ya heshima, nidhamu na kutii. Mahusiano haya pia huusisha mazingira bora ya kifamili, upendo nyumbani na katika jamii kwa ujumla na mambo mengine muhimu kama vile mawasiliano na mafundisho bora.

Waswahili wanasema ‘Asiye funzwa na mamaye, hufunzwa na ulimwengu”. Vitabu vya maadili ya kidini na afya ya jamii vinatangaza waziwazi kuwa msichana au mvulana yeyote anayepuuza wajibu wake wa msingi wa kuheshimu wazazi wake, atapata laana katika maisha yake. Neno laana humaanisha kuwa maisha yake yatakuwa ya kumwaibisha na kuiaibisha jamii. Na kwa sababu hiyo atakabiliwa na wakati mgumu katika maisha kama adhabu kali kutokana na kupuuza kanuni za maisha

Heshima kwa wazazi wa kambo

Wazazi wa kambo ni wazazi wanaobeba jukumu kwa niaba ya wazazi wa kibaiolojia. Vijana wanaolelewa na wazazi wa kambo wanatakiwa kufuata taratibu za kifamilia za wazazi hawa. Kutii na kuheshimu wazazi hawa huongeza afya, upendo na ustawi wa vijana. Dharau na kukosa adabu kwao huleta madhara zaidi kuliko mafanikio na ustawi wa kihisia na afya.

Upo wakati ambapo huenda wazazi hawa wakaonyesha mapenzi zaidi kwa ndugu wengine kuliko wengine na wakati mwingine wakaonyesha udhaifu wao katika malezi. Wazazi wakati mwingine huonekana kupendelea baadhi ya watoto kuliko wengine, hii hutokana na tofauti za msingi za watoto. Watoto ni binadamu na wanatofauti zao ambazo huwa msingi wa kupendwa zaidi kuliko wengine.

Ingawa si jambo jema kwa mzazi kuonyesha upendeleo kwa baadhi ya watoto kuliko wengine, lakini hili likitokea msichana anatakiwa kulikabili kwa moyo mweupe na hisia chanya kama changamoto na siyo kama tatizo la maisha.

Hili lisiwe jambo ambalo linamsononesha kijana anayelelewa na wazazi wa kambo. Udhaifu huo wa wazazi wa kambo unaweza kuonyeshwa pia na wazazi wa kibaiolojia. Vijana inawapasa kuelewa kuwa hakuna wazazi wakamilifu, wao nao ni binadamu na wakati mwingine wanakosea.

Jambo la msingi kwa vijana ni kukumbuka, kuwa hata pale wanapofikiri kuwa wazazi au watu wazima wamekosea, bado vijana wanawajibika kuonyesha heshima na moyo wa uvumilivu. Wanatakiwa kuwasilisha maoni na malalamiko yao kuhusu mambo wanayofikiri kuwa hayaendi vizuri, kwa njia bora za mawasiliano zinazodumisha afya ya kijamii na kihisia. Na kwa kufanya hivyo watawasaidia wazazi wao kujirekebisha. Kumbuka ni busara kuushinda ubaya kwa kutumia siraha ya wema.

Vijana wanaopitia katika mchakato wa “kukuwa kwa nguvu za kufikiri”, wanahitaji kuongozwa na kanuni bora za maadili ili kufanikisha ukuaji salama wa mwili na akili. Inawapasa wasichana kukumbuka kuwa usichana ndicho kipindi muhimu sana cha kufanya matayarisho ya kuwa mwanamke bora na mwenye mafanikio ya kiafya, kiuchumi na kijamii katika siku za baadaye.

Usichana ni fursa ikitumiwa vizuri mafanikio yatapatikana, lakini fursa hii ikitumiwa vibaya, hasara kubwa itatokea katika kipindi chote cha maisha. Maisha yatapoteza maana na kugeuka kuwa safari ya kuelekea kaburini bila kutimiza wajibu tuliopewa kwa njia ya kuzaliwa hapa duniani. Hakuna sababu ya kujuta hapo baadaye kama sasa unaitumia vibaya fursa ya usichana uliyopewa. Wapo wasichana ambao kujirahisisha na kuitumia vibaya miili yao bila kujali afya na maisha yao ya baadaye.

Siri za kuwa karibu na wazazi

• Fanya urafiki na wazazi au walezi wako, baba na mama ndio wawe rafiki zako wa kwanza tena wa karibu katika maisha yako. Washirikishe pia juu ya urafiki wako kwa wengine. Hii itakusaidia kuchota busara na uzoefu wao katika maisha.

• Tafuta muda wa kuongea nao hata kama wanashughuli nyingi, waonyeshe kuwa unalo hitaji la dhati la kuongea nao. Usiongee nao wakati wamechoka au wakiwa na hasira. Subiri muda ambao akili yao imetulia. Ongea nao kuhusu mambo yanayothaminiwa katika familia na jamii yenu, mipango ya familia na masomo yako. Waulize kuhusu mila na desturi za kabila lenu. Ongea nao kuhusu matukio muhimu ya familia, waulize wazazi kuhusu mabadiliko ya kibaiolojia ya mwili wako.

• Waulize wazazi wako kuhusu hasara za ngono na mimba za utotoni. Waulize juu ya miziki na vipindi vya luninga [TV] vinavyofaa kwa umri wako. Ongea nao kuhusu usafi wa nyumbani na mipango ya kuwasaidia kazi.

• Iga maisha mazuri ya wazazi na watu wa familia yako. Kwa ujumla msichana mwenye bidii ya kazi, utii, adabu na heshima njema ni fahari ya wazazi na kwa sababu hiyo wazazi watampenda, watamwamini, watamtegemea na kumheshimu sana. Hali hii itaongeza ubora wa maisha kwa kukujengea moyo wa kujiamini na kuthamini mambo yenye thamani maishani.

• Kumbuka kuwa wazazi wako ndio waalimu wa kwanza katika maisha yako. Jifunze kutoka kwao kwa kuangalia na kuiga mambo mazuri wanayofanya kila siku. Jifunze pia kutambua mambo mabaya wanayoyafanya na uyaepuke katika maisha yako. Kama unagundua kuwa hali duni ya maisha katika familia yenu inatokana na uvivu, ugomvi au ulevi wa wazazi, hii ni fursa nzuri kwako kujifunza athari na ubaya wa tabia hizo na kuziepuka.

Wazazi wanapokuadibisha

Wazazi wanapokukanya, kukuadhibu au kukutia adabu usione kuwa wanakuonea, kufanya hivyo ni jitihada za wazazi kukuonyesha kuwa wanakupenda na hawataki uharibikiwe katika maisha yako ya siku za usoni. Wazazi wanaokukanya wanakupenda wewe ila wanachukia makosa unayoyafanya.

Adhabu ya mzazi kama itazingatia haki za binadamu ni sehemu ya mapenzi yake kwa mtoto [6]. Adhabu ya mzazi anayekupenda ni faida ya roho yako kijana, anajaribu kukuokoa na mauti, anajaribu kulinda jina lako lisioze na kunuka vibaya katika jamii.[7]

Ingawa adhabu mara nyingi si njia bora ya kuwajenga vijana kitabia, wazazi wengi bado wanaitumia, njia hii isipotumika kwa busara adhabu inaweza kuchochea chuki, uasi na kulipiza kisasi. Vijana inawapasa kutii maagizo ya wazazi na kuwa wanyoofu kadri inavyowezekana ili kuepuka adhabu, mabishano na misuguano ya kifamilia.

Kwa upande mwingine wazazi wanaowaona vijana wakifanya makosa na kukaa kimya bila kuwakemea na kuwaonya, wanadhuru vibaya sana afya ya vijana wao kiakili, kiroho, kimwili na kijamii.