May 3, 2018

Huduma ya kwanza kwa mtu aliyeng’atwa na nyoka.

Nyoka ni wanyama hatari pale wanapomg’ata mtu, wanaweza kusababisha kifo papo hapo au baada ya muda.

Dalili anazopata mtu baada ya kung’atwa na nyoka hutegemea na aina ya nyoka.Kuna aina za nyoka ambazo huleta dalili papo hapo, na aina nyingine ambazo dalili huchelewa kujitokeza.

Kwa ujumla mtu anaweza kupata dalili zifuatazo:
 1. Kutokwa na damu, hasa sehemu aliyong’atwa.
 2. Maumivu sehemu aliyong’atwa
 3. Kupumua kwa tabu
 4. Ngozi kubadilika rangi, hasa sehemu aliyong’atwa
 5. Kuvimba sehemu au mguu uliong’atwa
 6. Mwili kuchoka na kukosa nguvu
 7. Kichefuchefu na kutapika
 8. Degedege
 9. Kutoona vizuri
 10. Kizunguzungu

Mtu aliyenga’twa na nyoka anahitaji kuwahishwa kwenye kituo cha afya haraka! Wakati utaratibu wa kumpeleka hospitali ukifanyika ni muhimu kumpa huduma ya kwanza.

Huduma ya kwanza
 1. Hakikisha mgonjwa anatulia, asihangaike wala kutembea tembea.
 2. Mlaze chini. Asiinue sehemu iliyong’atwa juu zaidi ya usawa wa moyo. Hii itasaidia kupunguza sumu kusambaa mwilini.
 3. Ondoa vitu vinavyobana kama pete au nguo za kubana kwenye sehemu iliyong’atwa kwani sehemu hiyo inaweza kuvimba
 4. Angalia hali ya mgonjwa: joto la mwili, mapigo ya moyo na upumuaji. Kama anakuwa wa baridi malze chali na kisha umfunike kwa blanketii
 5.  Muwahishe kituo cha afya
 6. Kama nyoka aliyemng’ata yupo (amekufa) nenda naye hospitali pia.

Wakati wa kutoa kuduma ya kwanza zingatia yafuatayo:
 1. Usifunge sehemu ya juu au chini ya alipong’atwa kwa kamba, nguo au kitu chochote.
 2. Usiweke barafu kwenye kidonda
 3. Usijaribu kunyonya sumu kutoka kwenye kidonda kwa mdomo
 4. Usikate au kupasua kidonda kwa kiwembe au kisu
 5. Usimpe kitu chochote cha kula
 6. Usiinue sehemu iliyong’atwa zaidi ya usawa wa moyo wa aliyeng’atwa.
 7. Muwahishe mgonjwa kwenye hospitali iliyo karibu na wewe ili apate matibabu na uangalizi.