May 15, 2018

Kulala chali kwa mjazito ni hatari kwa mtoto - Utafiti.

Wanawake wajawazito wanaopenda kulala chali wapo kwenye hatari ya kuzaa mtoto mfu (stillbirth), kulingana na wanasayansi.

Katika utafiti uliofanyika nchini Ghana, wanawake wajawazito ambao walipenda kulala chali wakati wa ujauzito walikuwa kwenye hatari mara tano zaidi ya kuzaa watoto wenye uzito mdogo na kwa wanawake wengine walizaa watoto wafu.

Utafiti huu ulifanyika nchini Ghana kutokana na kuwa kati ya watoto 1000 wanaozaliwa 20 hadi 50 kati yao huwa ni watoto wafu. Hata hivyo, utafiti mpya uliofanyika nchini New Zealand pia umehusisha kulala chali kwa mwanamke mjamzito na idadi kubwa ya watoto wafu wanaozaliwa katika nchi zenye raia wenye kipato kikubwa.

Mkuu wa utafiti huu, Louise O'Brien kutoka chuo kikuu cha Michigan, nchini Marekani amesema kama kutokulala chali wakati wa ujauzito hupunguza uwezekano wa kuzaa mtoto mfu basi ni vizuri kuhamasisha kina mama wajawazito kutolala chali kwani hii ni njia rahisi na isiyokuwa na gharama yoyote ile. Tabia hii ya kulala chali wakati wa ujauzito inaweza kuepukika kwa kuwashauri kina mama wajawazito madhara yanayopatikana kwa kulala chali.

Utafiti huu uliofanyika nchini Ghana unaunga mkono utafiti uliofanyika hivi karibuni nchini Australia unaojulikana kama Sydney Stillbirth Study ambao ulisema ya kwamba wanawake wanaolala chali wakati wa ujauzito wako kwenye hatari ya mara sita zaidi ya kuzaa watoto wafu.

Utafiti huu wa Australia ulifanyika kwa miaka mitano na ulihusisha wanawake wajawazito 295 kutoka katika hospitali nane nchini Australia. Naye mtafiti mkuu katika utafiti huu Dr. Adrienne Gordon, kutoka Sydney's Royal Prince Alfred Hospital amesema “Tafiti za awali zilionyesha ya kwamba wanawake wanaolala chali wakati wa ujauzito, hupunguza mzunguko wa damu unaotakiwa kwenda kwa mtoto.Lakini pia ni vizuri kwa wanawake ambao ni wajawazito kutotaharuki kama wakati mwingine watalala chali.’’